Prime
Ziara ya Samia India yaineemesha Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
- Ziara ya siku tatu ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India imeleta neema katika sekta za afya, elimu, kilimo na biashara, huku kukiwa na matumaini ya ajira mpya zitakazotokana na uwekezaji katika sekta hizo.
Dar es Salaam. Ziara ya siku tatu ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India imeleta neema katika sekta za afya, elimu, kilimo na biashara, huku kukiwa na matumaini ya ajira mpya zitakazotokana na uwekezaji katika sekta hizo.
Akitoa tathmini ya ziara hiyo iliyotokana na mwaliko wa Rais wa India, Droupadi Murmu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus alisema mbali na kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili, imeleta ushirikiano wenye tija katika maeneo ya kimkakati.
Katika sekta ya afya, alisema ziara hiyo imefanikisha kusainiwa mikataba itakayowezesha kujengwa viwanda vya dawa nchini na kuboreshwa huduma za afya kupitia ushirikiano kati ya wataalamu wa hospitali kubwa za India na Tanzania.
Mbali na hilo, pia taasisi ya Apollo yenye mtandao wa hospitali 73 nchini humo imekubali ombi la Serikali ya Tanzania kufungua tawi lake nchini, ili kusogeza huduma inazotoa karibu na Watanzania.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema katika ziara hiyo ilisainiwa hati na mikataba ya ushirikiano na hospitali kubwa nchini India kwa ajili ya kuwajengea uzoefu wataalamu wa ndani katika matibabu ya kibingwa.
“Tumesaini hati ya makubaliano na taasisi ya Max BLK yenye mtandao wa hospitali kadhaa nchini India kwa ajili ya upandikizaji ini na hatua ya pili ya upandikizaji figo, wataalamu wetu watajifunza kutoka kwao na wao watatuletea wataalamu. Pia tumesaini hati ya makubaliano na hospitali ya watoto ya Rainbow, hawa wamebobea katika matibabu yote ya watoto ya kibingwa.
Waziri huyo alisema wamepata mwekezaji ambaye yuko tayari kuwekeza kwenye uzalishaji wa dawa nchini, kwa kuwa asilimia 80 ya dawa zote zinazotumika nchini zinatoka nje ya nchi na asilimia 60 ya hizo zinatoka India. Hivyo kuwaleta wawekezaji katika eneo hilo ni hatua kubwa,” amesema.
Hatua hiyo, waziri alisema itawezesha kupungua kwa gharama za dawa na upatikanaji wake utakuwa wa uhakika, tofauti na ilivyo sasa ambapo zinaweza kusubiriwa kwa miezi tisa.
Uzalishaji wa dawa utakaofanyika nchini utakuwa sehemu ya kongani ya viwanda kutoka India, ambayo inatarajiwa kujengwa nchini, Ummy amesema.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba alisema mojawapo ya maeneo ya makubaliano kati ya mataifa hayo, ni India kuanzisha kongani itakayokuwa na jumla ya viwanda 200 vya bidhaa mbalimbali.
“Itakuwepo kongani ya viwanda, tayari eneo la ekari 1,000 limepatikana kule Pwani, kati ya hivyo vitakuwepo vinavyohusika na uzalishaji wa dawa, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na uundaji wa vifaa na teknolojia zinazotumika kwenye kilimo.
“Serikali imekubaliana na kampuni za matrekta za Mahindra na John Deer kuwekeza katika kipindi cha miezi 12, viwanda vya kuunganisha matrekta na kutengeneza vipuri ndani ya Tanzania,” amesema Makamba.
Katika sekta ya kilimo ziara hiyo imefanikisha kupata uhakika wa soko la mbaazi ambapo Rais Samia aliomba kupatiwa soko la tani 200,000 kwa kuwa India ni mtumiaji mkubwa wa zao hilo duniani.
Tanzania inakuwa nchi ya tatu Afrika kupata fursa hiyo ya mgawo kutoka India, sambamba na Malawi na Msumbiji ambazo pia zinazalisha mbaazi.
Akizungumzia hilo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema kupata soko hilo ni hatua kubwa, ikizingatiwa kwamba India ni watumiaji na wazalishaji wakubwa wa mbaazi.
“Tanzania inaingia kwenye ramani ya nchi ambazo tuna makubaliano nao ya kuwauzia mbaazi, kazi kubwa imefanyika kuhakikisha tunafikia hatua hii. Mbaazi kwa India ni siasa, maana hata wao wanazalisha kwa wingi, hivyo kuruhusu sisi tuingize tuna kila sababu ya kushukuru uhusiano huu.
“Niwahakikishie Watanzania hatuna tatizo na ubora wa mbaazi zinazozalishwa nchini, hata ukilinganisha na hizo za Malawi na Msumbuji ubora wa mbaazi zetu uko juu. India wanatumia wastani wa tani milioni tano za mbaazi kwa mwaka na uzalishaji wao hauzidi tani milioni nne,” amesema Bashe.
Kwa mwaka jana, Tanzania ilizalisha tani 108,222 na mwaka huu inatarajia kuzalisha zaidi ya tani hizo, hii ni kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo.
Katika eneo hilo la kilimo, pia Serikali iliwasilisha uhitali wa dola bilioni moja (Sh2.5 trilioni) kutoka Benki ya Exim ya India kwa ajili ya mradi mkubwa wa umwagiliaji kutoka Ziwa Victoria ambao utekelezaji wake utahusisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora, Dodoma, Kagera na Mara.
“Lengo la Serikali ni kufikia mwaka 2030 tuwe na kilimo cha umwagiliaji katika eneo la hekta milioni nane, mwaka huu tutafika hekta 1.2 milioni, hadi kufikia 2025 tutafikia hekta 1.5 milioni. Ni vizuri tukaelewa kuwa miradi ya umwagiliaji ina gharama kubwa na inahitaji teknolojia za kisasa. Kipaumbele chetu katika kilimo cha umwagiliaji ni mazao ya chakula,” amesema Bashe.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema mradi wa maji wa Ziwa Victoria utasaidia kuongeza uhakika wa upatikanaji wa maji katika mikoa iliyotajwa.
Kuhusu Dodoma ambayo itakuwa miongoni mwa wanufaika wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, Aweso alisema lengo ni kuondoa tatizo lililojitokeza baada ya Serikali kuhamia kwenye mkoa huo na mahitaji kuongezeka.
“Kabla Serikali haijahamia Dodoma, mahitaji ya maji yalikuwa lita milioni 44 na mamlaka yao ya maji ilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 61, kwa sasa mahitaji ni lita milioni 140, hivyo tunapambana kuondoa tatizo hilo,” amesema Aweso.
Maeneo mengine yaliyoingiwa makubaliano ni uimarishaji wa masuala ya kidijitali, ushirikiano wa masuala ya kiutamaduni, ujenzi na ukarabati wa vyombo vya majini huku Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kikisaini makubaliano ya kushirikiana na taasisi ya India.
Kwa upande wa sekta binafsi, Chemba ya Biashara ya Viwanda na Kilimo imeingia takriban makubaliano matatu na India na Chemba ya Biashara ya Zanzibar nayo imeingia makubaliano na Chemba ya chakula na Kilimo ya India.
Miongoni mwa hati za makubaliano zilizosainiwa ipo ya kushirikiana katika masuala ya White Shipping, yaani kubadilishana taarifa kuhusu meli, kuhakikisha kuna usalama majini na utulivu katika eneo.