Zelothe kuzikwa Jumatatu Arusha

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen enzi za uhai wake
Muktasari:
- Wanachama wa CCM Mkoa Arusha kupokea mwili wa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa Arusha kesho Uwanja wa Ndege Arusha.
Arusha. Mwili wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa Arusha, Zelothe Stephen aliyefariki dunia jana jijini Dar es Salaam unatarajiwa kupokewa kesho saa tisa jioni Uwanja wa Ndege Arusha.
Baada ya mwili huo kupokewa na wanaCCM utapelekwa Hospitali ya Mkoa Arusha ya Mount Meru na atazikwa Jumatatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 27, 2023 , Ofisi za CCM Mkoa Arusha, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa Arusha, Seipulani Ramsey amesema wanaomba wakazi wa Mkoa Arusha kujitokeza kupokea mwili wa mwenyekiti mkoa.
"Tunaomba wanaCCM wote Mkoa wa Arusha kujitokeza uwanja wa ndege kupokea mwili wa mwenyekiti wetu na Jumatatu kuja katika mazishi," amesema.
Amesema mazishi yatafanyika Jumatatu, nyumbani kwake Kata ya Olorieni, tawi la Olosiva wilayani Arumeru Mkoa Arusha.
Ramsey amesema anaomba wana CCM kuendelea kuwa wamoja na watulivu kipindi hiki kigumu.
"Tuendelee kumuenzi Mwenyekiti wetu alipenda sana umoja na ushirikiano alichukia Makundi na alikuwa nguzo kubwa ya CCM Mkoa Arusha," amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa Arusha, Moses Adam amesema Zelothe atakubukwa kwa kuwaunganisha wanaCCM Mkoa Arusha.
"Zelothe alikuwa ni kiongozi mkweli, alikuwa hapendi makundi na alikipenda sana chama chetu alichukia makundi hatujuwi baada ya kifo chake hali itakuwaje Arusha," amesema.
Zelothe kabla ya kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa Arusha aliwahi kuwa Kamanda wa Polisi mikoa kadhaa nchini na Mkuu wa Wilaya Musoma na baadaye kustaafu.