Zaidi ya watoto 400, 000 kupata matone ya Vitamini A

Ofisa Lishe Mkoa wa Mara, Benson Sanga akizungumza juu ya kampeni ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Zaidi ya watoto 468, 000 wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Mara wanatarajiwa kupatiwa matone ya Vitamini A katika kampeni ijulikanyo kama Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto.
Musoma. Zaidi ya watoto 468, 000 wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Mara wanatarajiwa kupatiwa matone ya Vitamini A katika kampeni ijulikanyo kama Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto.
Matone hayo ya vitamin A yatatolewa katika vituo 316 vya huduma za afya mkoani Mara kuanzia Juni Mosi, 2023 hadi Juni 30, 2023.
Akitoa taarifa mjini Musoma leo Mei 31, 2023 wakati wa kikao cha Afya ya Msingi Mkoa wa Mara, Ofisa Afya Mkoa wa Mara, Benson Sanga amesema kampeni hiyo pia itahusisha utambuzi wa hali ya lishe kwa watoto.
"Mkoa Mara bado haufanyi vizuri katika utoaji wa matone ya vitamini A baada ya asilimia nane pekee ya watoto 450, 000 waliolengwa kufikiwa ndio walipatiwa vitamin A. Mwaka huu tumepanga kuwafikia walengwa wote," amesema Sanga
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Helen Keller International (HKI), Dk Deogratias Damas amesema shirika hilo itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wote kufanikisha kampeni hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema tayari uongozi wa wilaya hiyo umeweka mikakati kufanikisha watoto wote wenye sifa wanapatiwa matone ya vitamini A.