Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanayokwamisha ubiasharishaji bunifu, tafiti

Muktasari:

  • Ubiasharishaji wa tafiti na bunifu ni mchakato mpana unaohitaji mazingira bora, ufadhili wa kutosha, ushauri wa kimkakati na ushiriki wa sekta binafsi.

Dar es Salaam. Ukosefu wa rasilimali fedha, uhusiano hafifu na sekta ya viwanda, na upungufu wa miundombinu ya biashara vimetajwa kama vikwazo katika ubiasharishaji wa utafiti na bunifu mbalimbali zinazofanyika nchini.

Hayo yamebainishwa leo Machi 29, 2025 jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye katika hafla ya kufunga warsha ya siku nne kuhusu ubisharishaji wa tafiti.

Anangisye amesema ubiasharishaji wa tafiti na bunifu ni mchakato mpana unaohitaji mazingira bora, ufadhili wa kutosha, ushauri wa kimkakati na ushiriki wa sekta binafsi.

"Pengo kati ya tafiti za vyuo na utekelezaji wake kwenye sekta ya viwanda na biashara ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa dhati kati ya Taasisi za Elimu ya Juu, Sekta Binafsi, Serikali na Wawekezaji"


"Hili ndilo linalotufanya tuweke mkazo mkubwa kwenye ushirikiano kati ya Chuo na Tasnia (yaani Academic-Industry Linkage)"anasema.

Amesema lengo  ni kuhakikisha kwamba bidhaa zetu za ubunifu zinaingia sokoni, zinatengeneza ajira, zinaboresha maisha ya Watanzania, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Taifa letu.

Ameongeza kuwa ili kufikia malengo hayo amewasihi  wadau  wa sekta binafsi na wawekezaji kuendelea kushirikiana na watafiti,  kutoa  ushauri na mitaji itakayosaidia  kugeuza mawazo ya kibunifu kuwa biashara na huduma zenye tija kwa jamii.

"Kwa upande wa wabunifu  nawahimiza kuchukua fursa hii adhimu kujifunza, kushirikiana na wazalishaji, na kujipanga vyema katika mchakato wa kuingiza bidhaa zenu sokoni, Huu ndio wakati wenu wa kuonesha kuwa utafiti unaweza kubadilisha maisha"amesema.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Maajar amesema ni ngumu kufikia  mafanikio hayo  bila kuzingatia umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya fedha endelevu, usimamizi wa miliki bunifu (IP), na ulinganifu wa sera za kitaifa.

Maajar amesema mambo hayo ni muhimu ili kuvutia uwekezaji, kuhamasisha ujasiriamali na kuchochea ukuaji wa uchumi unaotokana na maarifa na teknolojia.

"Napenda kutumia nafasi hii kutoa rai kwa wadau wote Serikali, Wawekezaji, Washirika wa Sekta Binafsi, na Jumuiya ya Kitaaluma, kushirikiana nasi kwa dhati katika juhudi hizi"amesema.

Ameongeza kuwa mafanikio ya muda mrefu ya tafiti zinazofanyika yanategemea uwezo  wa pamoja wa kuzigeuza kuwa suluhisho madhubuti za changamoto zinazoikabili jamii.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema ni muhimu kwa wanataaluma kuendelea kufanya tafiti kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na kuja na namna sahihi za kuzitatua.

Hivyo ushirikiano kati yao, serikali na sekta binafsi ni muhimu ili kufanya ziweze kufanyika kwa viwango vya juu na kuleta manufaa kwa watumiaji.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha inawaibua na kuwawezesha watafiti pamoja na wabunifu nchini.

Pia kufanya urejeaji wa sera mbalimbali ili ziweze kuendana na wakati wa sasa.