Woga uliua uhuru wa wasomi kujieleza-Shivji

Profesa Issa Shivji akizungumza wakati wa kongamano lililoangazia uhuru wa wanataaluma jijini Dar es salaam. Picha na Elizabeth Edward
Dar es Salaam. Hofu dhidi ya Serikali ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuwa sababu ya kufifia kwa mijadala ya wasomi, jambo ambalo limetajwa kama kikwazo cha maendeleo ya nchi.
Hilo limejitokeza kwenye kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ndaki ya Sayansi ya Jamii (Coss), lililowakutanisha wanazuoni kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali barani Afrika.
Akizungumza kwenye kongamano hilo jana, Mwanazuoni mkongwe, Profesa Issa Shivji aliwataka wanataaluma kubadili hali hiyo na “kutimiza wajibu na jukumu lao” la kuendeleza mijadala yenye tija kwa nchi bila kuhofia chochote, kwa kuwa ili taifa liendelee lazima kuwepo mijadala.
Kauli ya mwanazuoni huyo aliyebobea katika sheria, inaakisi hali iliyokuwepo nchini miaka kadhaa iliyopita, kipindi ambacho haikuwa rahisi wasomi kufanya majadiliano kwa uhuru.
Katika kipindi hicho, Serikali ilitangaza zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, jambo lililotajwa kuwa kikwazo cha demokrasia na mbinu ya kubana mianya ya uhuru wa kujieleza.
Bila kufafanua kipindi hicho, Profesa Shivji alisema “kuna wakati ambapo kulikuwa na hofu nyingi kwenye chuo hiki (UDSM) kuzungumza au kujadili kwa sababu ya kuogopa kufuatiliwa. Kuna wakati wanafunzi wawili au watatu hawakuweza kukusanyika pamoja.
“Ilifikia hatua mtu hawezi kumwalika mwingine kwa ajili ya kutoa mhadhara, akisema ni lazima upate kibali, tukawa na jamii ya kibali. Kuandaa mhadhara uwe na kibali na useme nani atakuja na atazungumza nini na kwa nini.
Matokeo yake mihadhara na mijadala ilikufa,” alisema Profesa Shivji kwenye mjadala ulioshirikisha vyuo vikuu vya Makerere (Uganda), Nairobi na Kabarak (Kenya), Bujumbura (Burundi), Witswatersrand (Afrika Kusini) na Chuo Kikuu cha Rwanda.
Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu Ardhi, Dodoma, Muhas na UDSM vya Tanzania.
Kinyume na hali hiyo, msomi huyo alisema katika miaka ya 1970 hadi 1990 mijadala ya kitaaluma ndiyo iliyokuwa alama ya taasisi hiyo, lakini utaratibu huo ukabadilika.
Profesa huyo aliyebobea pia katika sayansi ya siasa, alisema licha ya wakati mwingine mifumo ya nchi kuwabana watu wasizungumze, wanataaluma wanapaswa kuendelea kupaza sauti bila woga kwa kuwa ni jukumu lao.
Hata hivyo, kauli hiyo inakuja katikati ya dhana kwamba wasomi wengine, licha ya kutishwa wameacha kuzungumza kwa uhuru si tu kwa woga, bali kwa kinachodaiwa kujiweka katika mazingira rafiki ya kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali za kisiasa.
Lakini, msomi huyo aliweka bayana kuwa ni muhimu kuuweka kipaumbele uhuru wa wanataaluma kwa kuwa wana mchango mkubwa katika utengenezaji wa sera na mipango mbalimbali katika nchi.
“Tumekuwa na vipindi mbalimbali katika chuo hiki na uhuru wa wanataaluma haukuwepo mara zote, mara nyingine sio kwamba uhuru ulibanwa, lakini wanataaluma wenyewe walijihisi wamebanwa na hivyo kuhofia kujadili. Niwakumbushe wanataaluma, mpo huru kuzungumza,” alisema.
Katika mjadala huo, uliolenga kuzungumzia mchango wa taasisi za elimu ya juu katika kuleta suluhu kwenye jamii, Profesa Shivji alisema uhuru wa taaluma ni muhimu na si sawa kuvidhibiti vyuo kama idara za Serikali.
“Wanataaluma wanapaswa kuwa huru kuzungumza bila hofu,” aliongeza.
Mtazamo wa kufifia kwa mijadala ya wanataaluma haukuwa wa Profesa Shivji pekee, hata kwa Mkuu wa ndaki ya Sayansi za Jamii chuoni hapo, Profesa Christine Noe aliyesema “mijadala iliyopo haina nguvu kama iliyokuwepo miaka 40 iliyopita.”
Hata hivyo, alisema kupitia kongamano hilo, wanazuoni watajitathmini na kujadiliana namna ya kuanzisha upya mijadala yenye tija kwa ajili ya kusaidia jamii na Serikali.
“Tumeona kama ndaki tukae kujadili nini kimetokea, lini tulianza kupoteza umuhimu wa kusikilizwa, tunaweza kufanya nini ili wanataaluma na wanazuoni wa sasa wawe kama wa miaka ya nyuma.”
Alisema wakati huo wanataaluma walikuwa wanashauri Serikali na walikuwa wanategemewa na hivyo wanataka warudi huko.
“Kupitia mkutano huu tutaangalia sisi wenyewe ni namna gani tunawajibika kwa jamii ya ndani na kimataifa. Tunataka kuwajulisha jumuiya ya sasa ya wanazuoni, kwamba tuna jukumu kubwa la kuhakikisha taaluma inaleta matokeo kwenye jamii,” alisema Profesa Noe.
Profesa huyo, aligusia suala la kuminywa kwa wanataaluma, ingawa alisema yeye anaamini kushauri ni jukumu lao na kwamba mwenye sababu za kisayansi anaweza kufanya hivyo na akasikilizwa.
“Ni kweli kuna kuminywa, lakini tunaamini kwamba wanataaluma na sisi tuna jukumu kwa sababu taaluma inafanyika kisayansi. Ukiwa na sababu za kisayansi na ukazitumia kushauri iwe kwa Serikali au jamii, lazima utasikilizwa,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wanataaluma kujadili kwa kuzingatia majukumu yao na kuacha kuegemea kwenye siasa kwa kuwa hilo ndilo linalochangia waonekane wameegemea upande mmoja.
Licha ya mjadala huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (taaluma) wa UDSM, Profesa Nelson Boniface alisema chuo hicho kinatoa uhuru kwa wanataaluma kuzungumza mambo yao kwa uhuru bila kuharibu wala kuvunja sheria za nchi.
“Wanataaluma wanajua kwamba kuna uhuru wa kujieleza na hilo ndilo linalofanyika hapa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wako huru kuzungumza mawazo yao bila kuvunja sheria na kanuni za nchi,” alisema Profesa Boniface.
Miongoni mwa waliohudhuria mjadala huo, ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema uwepo wa makongamo yanayojadili kuhusu uhuru wa kitaaluma ni muhimu si tu kwa vyuo vikuu, bali kwenye majukwaa yote.
“Majukwaa ya majadiliano ndiyo yanazalisha dhana. Wataalamu, wasomi na wanazuoni watabishana na kupata mambo ambayo yanaweza kuifanya jamii isonge mbele. Hii sio kwa Tanzania pekee, bali ni dunia nzima. Majukwaa ya mijadala ndiyo yanajenga mataifa, mataifa ambayo hayajadiliani hayawezi kusogea mbele,” alisema.
Mapema, Profesa Shivji alizindua toleo la pili la kitabu chake cha Dhana ya Haki za Binadamu kilichochambua jinsi zinavyotumikiwa na watawala wa dunia kufunika dhambi zao na si kuwashawishi watu kuendeleza mapambano yao ya kupata uhuru.