Wizara ya maji kuchunguza upatikanaji maji baridi Simiyu

Tenki la kuhifadhi maji lililojengwa na Ruwasa katika Kijiji cha Ipililo Wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga
Muktasari:
- Baadhi ya vitongoji vya Wilaya za Maswa na Meatu, zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, kwa kuwa yaliyopo katika maeneo hayo yana kiwango kikubwa cha chumvi.
Simiyu. Serikali kupitia wizara ya Maji imeahidi kutuma timu ya wataalamu na mitambo ya kisasa kufanya utafiti wa upatikanaji wa maji baridi katika maeneo yenye changamoto ya maji chumvi, hususan katika wilaya ya Maswa na Meatu mkoani Simiyu.
Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 5, 2025 na Mkurugenzi wa Raslimali za Maji, Wizara ya Maji, Dk George Lugomela wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ipililo wilaya ya Maswa baada ya kukagua mradi wa maji katika kijiji hicho.
Amesema kuwa Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama inazozikabili baadhi ya vijiji na vitongoji vya wilaya hizo, kwa kuwa maji yaliyopo katika maeneo hayo yana kiwango kikubwa cha chumvi.
“Kupitia wataalamu wetu, tutafanya utafiti wa kina ili kubaini vyanzo vya maji baridi vilivyoko chini ya ardhi. Tutatumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha tunapata maji salama na yenye ubora kwa matumizi ya binadamu,” amesema na kuongeza;
“Kupitia wataalamu wetu, tutafanya utafiti wa kina kubaini vyanzo vya maji baridi vilivyofichika chini ya ardhi. Tutatumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha tunapata maji bora kwa matumizi ya binadamu.”

Tenki la maji lililowekwa juu kwenye kituo cha kuchotea maji katika kijiji cha Ipililo. Picha na Samwel Mwanga
Ameongeza kuwa mitambo itakayotumika katika utafiti huo pia itajumuisha vifaa vya kuchunguza hali ya miamba chini ya ardhi, visima vya majaribio na teknolojia za kuchuja chumvi endapo itahitajika.
Dk Lugomela amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha, kila mwananchi anafikiwa na huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2030, sambamba na malengo ya maendeleo endelevu.
“Hii ni hatua muhimu kuelekea kutimiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za kijamii, hususan maji zinaimarika na kuwafikia wananchi wote mijini na vijijini,” amesema.
Mkazi wa kijiji cha Ipililo, Agnes Marco amesema kuwa licha ya kupatikana kwa huduma ya maji baada ya Serikali kujenga mradi mkubwa, lakini yamekuwa na kiasi kikubwa cha chumvi, hivyo kushindwa kuyatumia hasa kwa kunywa.
Dotto Salu ni mkazi wa kijiji hicho amesema wanapoyatumia maji hayo kwa ajili ya kuoga, husababisha mwili kuwasha na kupauka hali inayowalazimu kuacha kuyatumia na kwenda kutafuta kwenye vyanzo visivyo salama.
Dk Mathias John ni daktari wa ngozi mjini Maswa, amesema kuwa kutumia maji yenye kiasi kikubwa cha chumvi hasa kwa kuoga yakifika machoni husababisha kuchoma, kuwasha na macho kuwa mekundu.

Mkurugenzi Raslimali za Maji,Wizara ya Maji, Dk George Lugomela (mwenye kofia) akipitia taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Ipililo Wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga
“Mtu mwenye vidonda vya wazi, michubuko au majeraha, kuoga kwa kutumia maji yenye kiasi kikubwa cha chumvi kunaweza kusababisha maumivu makali na hata kuongeza hatari ya maambukizi, hasa kama maji hayo si safi,” amesema.