Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WHO yatoa onyo virusi vipya homa ya nyani

Muonekano wa viganja vya mkono vya mtu mwenye ugonjwa wa homa ya nyani. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kamati ya dharura imeitishwa kutokana na kusambaa kwa Mpox nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuwapo uwezekano wa kuenea zaidi kimataifa ndani na nje ya Afrika.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema virusi vya clades 1 vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox (homa ya nyani) vinavyosambaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) vimejibadilisha na kuibuka vingine vya clade 1b ambavyo husababisha ugonjwa mkali zaidi.

WHO imesema kwa miaka mingi clade 1 vimekuwa vikisambaa nchini DRC, huku clade 2 vilisababisha mlipuko kimataifa kuanzia mwaka 2022.

Shirika hilo limesema mlipuko wa sasa mashariki mwa DRC unasababishwa na kujibadilisha kwa virusi vya clade 1 na kuibuka vya clade 1b ambavyo husababisha ugonjwa mkali zaidi kuliko clade 2.

WHO imesema virusi vya clade 1b ndivyo vilivyothibitishwa Kenya, Rwanda na Uganda, wakati nchini Burundi uchunguzi unaendelea kufanyika.

Mbali ya hayo, WHO imesema mwaka huu kumeripotiwa taarifa za virusi vya clade 1 nchini DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Congo, wakati clade 2 imeripotiwa  Cameroon, Ivory Coast, Liberia, Nigeria na Afrika Kusini.

Kutokana na hayo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedross Ghebreyesus ameiita kamati ya dharura chini ya Kanuni za Afya za Kimataifa kumshauri, iwapo mlipuko wa sasa wa Mpox ni suala la dharura la afya ya umma linalohitaji kushughulikiwa kimataifa.

Ameiita kamati hiyo wakati ambao virusi hivyo vikisambaa nje ya DRC, na kuwapo uwezekano wa kuenea zaidi kimataifa ndani na nje ya Afrika.

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya WHO jana Agosti 7, 2024 imesema Dk Ghebreyesus ameagiza kamati hiyo ikutane mapema iwezekanavyo. Inahusisha wataalamu huru wa taaluma mbalimbali kutoka maeneo kadhaa duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk Ghebreyesus amesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu, DRC inakabiliwa na mlipuko wa Mpox, kukitolewa taarifa zaidi ya 14,000 kuhusu ugonjwa huo uliosababisha vifo vya watu 511.

Mlipuko wa Mpox umekuwa ukiripotiwa nchini DRC kwa miongo kadhaa, lakini idadi ya taarifa zimekuwa zikiongezeka kila mwaka kwa kasi ndogo.

Hata hivyo, idadi iliyoripotiwa katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2024, amesema inalingana na idadi ya taarifa iliyotolewa mwaka 2023, huku virusi vya ugonjwa huo vikisambaa katika majimbo ambayo hayakuathirika awali.

“Mwezi uliopita (Julai), takribani taarifa 50 zimethibitishwa kuwa ni Mpox na nyingine zinazohisiwa kuwa ni za ugonjwa huo zimeripotiwa katika nchi nne jirani na DRC ambazo hazijawahi kuripoti awali ni Burundi, Kenya, Rwanda, na Uganda,” amesema.

Shirika hilo limesema linafanya kazi na Serikali za mataifa hayo, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) Afrika, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), asasi za kiraia na washirika wengine katika kubaini, kushughulikia vinavyochochea mlipuko huo na kuzuia usambaaji.

WHO imeshauri kutoweka vikwazo vya kusafiri kwa nchi zilizoathirika, lakini kupitia kanda imeandaa mpango kusaidia shughuli za ufuatiliaji wa ugonjwa huo, ikieleza kuna chanjo mbili za Mpox zilizoidhinishwa na mamlaka ya udhibiti wa kitaifa iliyoorodheshwa na WHO.

“Nimeanzisha mchakato wa orodha ya matumizi ya dharura ya chanjo zote mbili, ambayo itaharakisha upatikanaji wa chanjo, hasa kwa nchi zenye kipato cha chini ambazo bado hazijatoa idhini ya udhibiti wa kitaifa,” amesema Dk Ghebreyesus.

Amesema orodha ya matumizi ya dharura pia inawawezesha washirika wakiwamo Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na upatikanaji wa chanjo (Gavi) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kununua chanjo kwa ajili ya usambazaji.


Serikali ya Tanzania

Tayari Serikali imetoa tahadhari kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa Mpox unaosambaa kupitia majimaji ya mwili, ikiwemo mate, matapishi, jasho na mkojo.

Kwa mujibu wa WHO, ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya Mpox unasambaa kwa njia za matone ya mfumo wa njia ya hewa, ngozi kupitia kugusa na kujamiana na mtu mwenye maambukizi. Pia ugonjwa huo unaenea kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.

Wizara ya Afya katika taarifa kwa umma iliyotolewa wiki iliyopita ilieleza hadi sasa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa aliyepatikana na ugonjwa huo ambao dalili zake ni upele, malengelenge au vidonda kwenye mwili hasa mikononi na miguuni, kifuani, usoni na wakati mwingine sehemu za siri.

“Dalili nyingine ni homa, maumivu ya kichwa, misuli, mgongo, uchovu na kuvimba mitoki. Ugonjwa huu haujaingia nchini, hivyo, ni vema tukashirikiana kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa salama,” imeeleza taarifa hiyoya wizara hiyo.

Kutokana na hilo, Serikali imewataka Watanzania kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kubusiana na mtu mwenye dalili za Mpox.

Serikali imewataka wananchi kuepuka kugusana na mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox na kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

Pia wametakiwa kuepuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni, kusafisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mhisiwa au mgonjwa pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara.

“Kuvaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox, kuwahi vituo vya huduma za afya unapoona dalili za ugonjwa wa Mpox. Watoa huduma za afya wanatakiwa wazingatie miongozo ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi (IPC) wakati wote wanapowahudumia wagonjwa,” imeeleza taarifa hiyo.