Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenza waliohukumiwa miaka 20 jela waibwaga Serikali, waachiwa huru

Muktasari:

  • Mahakama ya Rufani imetulipia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na DPP, ili Mahakama hiyo irejee uamuzi wake uliowaachia huru wanandoa hao, baada ya kutokea dosari za kisheria wakati wa upekuzi na ukamataji.

Arusha. Wamejinasua. Hili ndilo neno linaloweza kuelezea namna wanandoa Ayubu Mfaume na Pilly Mohamed walivyoponea chupu chupu kutupwa jela miaka 20 baada ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroini, kufuatia kuachiwa huru na Mahakama ya Rufani Tanzania.

Hii ni mara ya pili kwa wanandoa hao kumshinda Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika Mahakama ya Rufani.

Awali, walihukumiwa kifungo hicho na Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam, kupitia kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2019.

Kutoridhishwa na hukumu hiyo, wanandoa hao waliwasilisha rufaa Mahakama ya Rufani na Machi 11, 2022, katika rufaa ya jinai ya mwaka 2020, waliachiliwa huru.

Hata hivyo, DPP hakuridhika na uamuzi huo na aliwasilisha maombi ya marejeo katika Mahakama hiyo hiyo akitumia Kanuni ya 66(1)(a), (b) na (2) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009, akiomba uamuzi huo wa Machi 2022 upitiwe upya.

Mei 7, 2025, jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija, Patricia Fikirini na Sam Rumanyika lilitupilia mbali maombi hayo ya DPP na kuendeleza msimamo wa Mahakama hiyo kuwa upekuzi na ukamataji haukufuata taratibu za kisheria, hivyo ulikuwa batili.


Kuhusu kesi ya awali

Katika kesi hiyo, Ayubu na Pilly walifikishwa mahakamani na upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi sita. 
Miongoni mwao ni Inspekta Emmanuel Ambilikile (shahidi wa tatu), Raymond Kimambo (shahidi wa sita) na Neema Mwakagenda (shahidi wa nne). 
Mashahidi hao walidai kuwa Mei 23, 2018, saa mbili asubuhi,

walifanya upekuzi katika nyumba ya wanandoa hao iliyopo Tegeta Nyuki Masaiti, Wilaya ya Kinondoni na kukuta unga mweupe unaoshukiwa kuwa dawa za kulevya ukiwa kwenye mfuko wa nailoni nyeusi.

Shahidi wa tatu, ambaye kwa wakati huo alikuwa ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), alieleza kuwa alikuwa msimamizi wa timu ya upekuzi na alimkabidhi mfuko huo kwa shahidi wa nne kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Mashahidi wengine waliotoa ushahidi ni Inspekta Hassan Zahoro (shahidi wa pili), Shimo Peter (shahidi wa kwanza), na Inspekta Lubambe Kanyumbu (shahidi wa tano). 

Shahidi wa pili alieleza kuwa alipeleka sampuli kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo uchunguzi ulithibitisha kuwa kilichopatikana ni dawa za kulevya aina ya heroini.

Mahakama ilizingatia ushahidi wa pande zote mbili na ikaridhika kuwa mashtaka yalithibitishwa, hivyo ikawatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela kabla ya kuachiwa huru kwenye rufaa.


Rufaa ya kwanza

Baada ya hukumu ya awali, wanandoa Ayubu Mfaume na Pilly Mohamed walikata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo, wakitoa hoja saba za kupinga hukumu hiyo.

Miongoni mwa hoja hizo ni kuwa upekuzi uliofanyika nyumbani kwao haukuwa halali kwa mujibu wa Kifungu cha 38 (1), (3) na 40 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kwa kuwa ulifanyika usiku na bila hati ya upekuzi.

Upande wa mashitaka ulijibu kuwa upekuzi huo ulitekelezwa katika hali ya dharura, hivyo ushahidi uliopatikana ulikubalika chini ya Kifungu cha 42 cha CPA. 

Pia walidai kuwa hata kama isingekuwa hali ya dharura, ushahidi huo bado ungeweza kukubalika kwa mujibu wa Kifungu cha 169 cha sheria hiyohiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama ya Rufani ilibaini kuwa upekuzi huo uliofanywa na shahidi wa tatu haukufuata masharti ya kisheria, hasa kwa kutofanyika kwa kibali kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 38 (1) cha CPA. 

Mahakama ilisisitiza kuwa pamoja na kwamba maofisa wa DCEA wana mamlaka ya kufanya upekuzi na ukamataji. Mamlaka hayo ni lazima yatekelezwe kwa kuzingatia masharti ya CPA.

Kuhusu madai ya hali ya dharura, Mahakama ilieleza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 42(1)(a) na (b) cha CPA, upekuzi na ukamataji unaweza kufanywa bila hati katika mazingira ya dharura, lakini katika kesi hii, ushahidi haukuonesha kuwepo kwa hali hiyo ya dharura.

Kuhusiana na hoja ya upande wa mashitaka kuwa ushahidi ungeweza kukubalika chini ya Kifungu cha 169 cha CPA, Mahakama ilikataa hoja hiyo, ikisema kuwa ushahidi huo haukuhalalishwa kwa njia yoyote kisheria. Kutokana na hilo, Mahakama ilikubali hoja ya kwanza ya wanandoa hao na kuwaachia huru.


Rufaa ya DPP

Kutokana na uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, DPP hakuridhika na aliwasilisha maombi ya mapitio kwa mujibu wa Kanuni ya 66(1)(a) na (b) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009, yaliyoambatanishwa na hati ya kiapo.

Maombi ya DPP yaliegemea kwenye misingi miwili: kwanza, kuwa Mahakama haikuzingatia matakwa ya kisheria chini ya vifungu vya 32 na 48 vya Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya, ambayo haimlazimishi ofisa wa DCEA kuwa na hati ya upekuzi; pili, kuwa tafsiri ya Mahakama kuhusu mamlaka ya shahidi wa tatu kama afisa wa DCEA inazuia utekelezaji wa majukumu ya maofisa hao bila idhini ya ofisa polisi mfawidhi.

DPP pia alidai kuwa hakusikilizwa ipasavyo katika baadhi ya hoja na kuwa Mahakama ilishindwa kuthamini ushahidi mwingine muhimu uliokuwapo kwenye rekodi kabla ya kutoa uamuzi wake.

Katika usikilizaji wa maombi hayo, DPP aliwakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Sabrina Joshi, huku wanandoa hao wakiwakilishwa na Wakili Nehemia Nkoko.
Wakili Sabrina alieleza kuwa Mahakama ya Rufani ilikosea kusema kuwa upekuzi huo ulipaswa kufanywa kwa mujibu wa CPA, ilhali sheria mahsusi ya dawa za kulevya ambayo ni DCEA, inaruhusu upekuzi kufanyika wakati wowote, usiku au mchana, kwa mujibu wa Kifungu cha 32(7).


Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, jopo la majaji likiongozwa na Augustine Mwarija lilibaini kuwa madai ya DPP kuhusu kunyimwa haki ya kusikilizwa hayakuwa na mashiko, kwa kuwa hoja hizo zilihusu kupinga uhalali wa uamuzi uliotolewa, si kukosa fursa ya kusikilizwa.

Jaji Mwarija alieleza kuwa baada ya ushahidi wa shahidi wa tatu kuondolewa kwa kuwa ulipatikana kwa njia isiyo halali (upekuzi bila hati), Mahakama iliona ushahidi uliobaki haukutosha kuthibitisha kesi dhidi ya wanandoa hao.

Katika maelezo yake, Jaji Mwarija alisisitiza kuwa Mahakama ilitupilia mbali pia hoja ya dharura ya upekuzi, ikibainisha kuwa ushahidi haukuonesha hali yoyote ya dharura kama inavyotakiwa kisheria chini ya Kifungu cha 42(1) cha CPA.

Alisisitiza kuwa ingawa maofisa wa DCEA wana mamlaka ya kufanya upekuzi na ukamataji kwa mujibu wa vifungu vya 32 na 48 vya sheria yao, mamlaka hayo bado yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia masharti ya CPA, hasa kuhusu kupata hati ya upekuzi.

Hatimaye, Mahakama ilihitimisha kuwa maombi hayo ya DPP hayakuwa na msingi wa kisheria na kuyatupilia mbali rasmi.