Wenyeviti wa mitaa, watendaji wapewa jukumu la kufichua waharibifu wa vyanzo vya maji Mbeya
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Ufundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBEYA UWSA), Barnabas Konga akizungumza na wadau wa maji na viongozi mbalimbali wakati wa ziara ya kukagua vyanzo vya maji ikiwamo Nzovwe. Picha na Sadam Sadick
Muktasari:
- Katika kikao hicho, wadau na viongozi mbalimbali walifanya ziara ya kukagua na kuona miradi na vyanzo vya maji huku wakipongeza juhudi zilizofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBEYA UWSA) wakionesha matumaini ya kuisha kwa kero ya Maji.
Mbeya. Wakati Jiji la Mbeya likiendelea kusubiri kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Mto Kiwira unaotarajiwa kumaliza tatizo la upungufu wa maji, viongozi wa mitaa, watendaji na madiwani wamepewa jukumu la kubaini na kufichua watu wanaoharibu vyanzo vya maji na miundombinu ya usambazaji ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Hatua hiyo inakuja baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya (MBEYA UWSA) kubainisha kuwa takribani asilimia 30 ya maji yanayozalishwa hupotea kutokana na wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu, hali inayochangia kuendelea kwa changamoto ya huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa maji kilichoandaliwa na MBEYA UWSA, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomoni Itunda, amesema ulinzi wa vyanzo vya maji unahitaji ushirikiano wa viongozi wa ngazi za chini kwa kuhakikisha shughuli zote zinazohatarisha mazingira hayo zinakomeshwa.
"Hakikisheni hakuna shughuli zozote za kiuchumi na kijamii katika maeneo ya vyanzo vya maji. Wanaofanya hivyo wafichueni haraka ili hatua kali zichukuliwe," amesema.
Mbali na kuzuia shughuli katika maeneo ya vyanzo vya maji, Itunda amesema Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inaendelea kutekeleza mkakati wa kupanda miti milioni 2.5 kila mwaka ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kulinda vyanzo vya maji.
Amesema juhudi hizo ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kuwa endelevu kadri mahitaji ya wananchi yanavyoongezeka.
Katika hatua nyingine, ameupongeza uongozi wa MBEYA UWSA kwa juhudi za kuboresha huduma ya maji, huku akieleza matumaini kuwa uzalishaji utaongezeka kutoka lita milioni 74 za sasa hadi kufikia lita milioni 90 kwa siku baada ya kukamilika kwa miradi inayoendelea.
"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Kiwira ambao umefikia asilimia 56. Tunatarajia ukikamilika utaondoa changamoto kubwa ya maji katika Jiji la Mbeya," amesema.
Mkurugenzi wa Ufundi na Uzalishaji wa MBEYA UWSA, Barnabas Konga, amesema mamlaka hiyo kwa sasa inazalisha lita milioni 74 za maji kwa siku wakati mahitaji halisi ya wananchi yamefikia lita milioni 90.
Amesema pamoja na jitihada za kuongeza uzalishaji, changamoto ya wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu inaendelea kuathiri utoaji wa huduma.
"Chanzo cha Mto Nzovwe kinahudumia takribani asilimia 40 ya wananchi wa Mbeya, hivyo ni eneo ambalo halipaswi kuguswa na shughuli zozote za kilimo. Tunawashukuru wananchi wanaoendelea kushiriki kukilinda," amesema.
Katika kikao hicho, viongozi na wadau walitembelea baadhi ya vyanzo vya maji na miradi inayotekelezwa na MBEYA UWSA, ambapo walieleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa na kueleza matumaini kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa kero ya maji.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameitaka mamlaka hiyo kuboresha ratiba za mgawo wa maji wakati wakisubiri kukamilika kwa miradi mikubwa.
Mkazi wa Mbeya, Maria Mwazembe, amesema licha ya maboresho yanayoendelea, bado wananchi hukabiliwa na changamoto ya kukosa maji kwa muda mrefu bila taarifa za kutosha.
"Tunaambiwa kuhusu mradi wa Mto Kiwira, lakini bado hatujui utakamilika lini. Tunaomba mamlaka iboreshe ratiba za mgawo kwa sababu wakati mwingine tunalazimika kuamka usiku kutafuta maji," amesema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ruanda, Isaack Mwakubombaki, amesema ziara ya kutembelea vyanzo vya maji imeonyesha kazi kubwa inayofanywa na MBEYA UWSA, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda miundombinu hiyo.
"Tumeona kazi kubwa iliyofanyika. Tunaamini miradi hii ikikamilika itaondoa kero ya maji, lakini jukumu la kulinda vyanzo vya maji ni la kila mwananchi," amesema Mwakubombaki .