Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wengine 48 wasomewa kesi ya uhaini Kisutu, wamo mafundi na wafanyabiashara

Muktasari:

  • Mpaka sasa watu 288 wameshafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka ya kula njama na kutenda kosa la uhaini.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Nisha Ismail (31) na wenzake 47 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhaini inayotokana na maandamano yaliyozaa vurugu wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Mbali na Ismail, ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea, washtakiwa wengine ni Lawifu Ally(24) mkazi wa Buguruni Madenge, Mbaruku Mbaruku(27) mkazi wa Tabata Mtambani, Damas Saki(47) mkazi wa Bunju, Hamis Nakuvalila(25) mkazi wa Temeke kwa Aziz Ally na wengine 43.

Washtakiwa hao ambao walikamatwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wakihusishwa na maandamano hayo, wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo leo Jumanne, Novemba 11,  2025.

Kati ya washtakiwa 48, wapo wafanyabiashara 19, madereva bajaji na bodaboda 13, wajasiriamali wanne, mafundi wanne wakiwemo wa ujenzi, fundi umeme, fundi randa,  mwanafunzi, mwalimu na mbeba mizigo.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mawili ambayo ni kula njama na ya uhaini.

Wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru ameieleza mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, washtakiwa wote wanakabiliwa na kesi uchunguzi wa awali (PI).

Katika shtaka la kwanza, wakili Mafuru amedai washtakiwa wote, kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Wakili Mafuru amedai washtakiwa hao walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haijakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa  wamepelekwa rumande kutokana na kesi inayowakabili haina dhamana.

Kuanzia Novemba 7, 2025 hadi leo, tayari washtakiwa 288 wameshafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa kesi ya uhaini.