Waziri Sangu aipa kibarua taasisi ya Uongozi

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deus Sangu akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Uongozi (hawapo pichani) wakati wa kikao chake cha kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanyakazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam jana Agosti 16, 2024.
Muktasari:
- Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema maendeleo yanayofanywa na Serikali yanapaswa kuungwa mkono kwa kuwa na bodi zenye weledi wa kuongoza mashirika.
Dar es Salaam. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ameitaka Taasisi ya Uongozi, kuweka kipaumbele kwenye mafunzo yanayohusisha wajumbe wa bodi za mashirika ya umma ili kujenga uelewa mpana wa masuala ya uongozi ili wazingatie maslahi ya Taifa.
Sangu ametoa rai hiyo jana Agosti 16, 2024 jijini Dar es salaam alipofanya ziara ya kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanya kazi na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi.
“Nimefarijika sana kusikia kuwa Taasisi ya Uongozi inatoa mafunzo mahususi ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji viongozi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania ikiwa pia ni sehemu ya utekelezaji wa jitihada za kuimarisha utawala bora,” amesema.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada za kujenga nchi katika nyanja mbalimbali, hivyo kuna haja ya kumuunga mkono kwa kufanya mafunzo yanayoweza kuwafanya viongozi mbalimbali kuwa wazalendo na wenye kiu ya kuona Taifa linapata maendeleo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deus Sangu akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Uongozi wakati wa kikao chake cha kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanyakazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ikulu, Majula Mahendeka na kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo
Vile vile, amesisitiza watumishi wa taasisi hiyo kuendelea na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa jukumu la kutoa mafunzo kwa Viongozi ni kubwa na linahitaji mshikamano.
Sangu amefanya ziara katika Taasisi ya Uongozi kwa kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu ya Taasisi hiyo ambayo ipo chini ya Ofisi anayoiongoza.
Akizungumza awali wakati wa kumkaribisha Waziri Sangu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Majula Mahendeka alimkaribisha Naibu Waziri huyo na kumhakikishia ushirikiano wakati wote utakapohitajika kwa kuwa yeye ndiye amsimamizi wa Sera.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo amesema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya Uongozi kwa makundi yote bila ubaguzi na kufanya utafiti wenye tija kwa jamii.
"Taasisi ya Uongozi imechangia kwa kiwango kikubwa uwezo wa reli ya kisasa (SGR) kwa kuwa kilipewa kazi ya kufanya utafiti kuhusu athari za uwepo wa reli hiyo kwa wananchi, hivyo tutafanya tena kujua manufaa kwa sasa ambapo treni hiyo ya mwendo kasi inafanyakazi," amesema Singo.