Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sangu: Serikali kutoa ajira kupunguza tatizo la upungufu watumishi nchini

Rukwa. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema Serikali imepanga kutangaza jumla ya  ajira mpya  37, 616 huku ajira za kada ya ualimu, afya  na kada nyinginezo ikiwemo kada ya uhasibu  na ugavi zikiwa tayari zinaendelea kutangazwa lengo likiwa ni kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi nchini.

Sangu ameyasema hayo leo Agosti 5, 2024 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Kitete, Laela, Kamsamba na Kavifuti vilivyopo katika  Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ikiwa ni ziara yake ya  kwanza tangu alipouteliwa kushika  wadhifa huo.

Akizungumzia nafasi za ajira ya ualimu ambazo tayari zimeshatangazwa na Sekretarieti ya Ajira kwenye ngazi ya mikoa kulingana na mahitaji ya mkoa husika, Sangu amesema utaratibu wa kuwapata walimu kwa mwaka huu umeanza kuwa wa tofauti ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Amefafanua kuwa usaili huo umeanza kufanyika kwa kada ya ualimu kwa sababu nafasi za ajira za ualimu  ni chache ukilinganisha na idadi ya walimu wa shule ya msingi na sekondari waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini ambapo zaidi ya walimu 100,000 wapo mtaani wakiwa hawana ajira.

Amesema Serikali imekuja na uamuzi huo ili kuchagiza dhana ya ushindani kwa lengo la kuhakikisha kila mwenye sifa stahiki anapata ajira katika mazingira aliyopo pasipo kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya usaili.

Kufuatia hatua hiyo Sangu ametoa wito kwa vijana waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini kuchangamkia nafasi hizo za ajira huku akiwataka wajiandae ipasavyo kwa ajili ya usaili huo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kada hiyo ya ualimu kufanya usaili

Ametumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi wote walioomba nafasi hizo za ualimu huku akiwahakikishia kuwa Ofisi yake yenye dhamana ya kusimamia masuala ya ajira nchini imejizatiti kuhakikisha mchakato huo wa kuwapata walimu wenye sifa stahiki utakuwa wa huru na haki.

“Katika kumsaidia Waziri wangu George Simbachawene tutahakikisha sera ya ajira nchini inayosisitiza haki ya kupata ajira bila kujali hali ya kiuchumi, rangi, kabila na dini inazingatiwa kikamilifu.” Amesema Sangu