Waziri Nape ashangazwa kupungua habari za uchunguzi

Muktasari:
- Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amevitaka vyuo na taasisi zinazotoa taaluma ya uandishi wa habari kufanya tathmini ya mchango wao katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari.
Dar es Salaam. Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amevitaka vyuo na taasisi zinazotoa taaluma ya uandishi wa habari kufanya tathmini ya mchango wao katika kukuza na kuendeleza tasnia ya habari.
Amesema tathmini hiyo ambayo inapaswa pia kuhusisha wadau wa habari itasaidia kujua mahitaji ya wanataaluma wanaohitajika kwenye soko.
Nape ameyasema hayo leo Jumatano Juni 29, 2022 wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya miaka 60 cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lililolenga kuangalia mchango wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC).
Akizungumzia hilo, Nape amesema tathmini na makongamano ya aina hiyo yatasaidia kuona uhitaji uliopo mtaani na kufanya mabadiliko ya mitaala kulingana na uhitaji.
“Hili ni jambo kubwa linalojenga utamaduni wa kufanya tathmini na kuchambua mapungufu yaliyopo katika mfumo wa kuwandaa wanahabari.
“Majukumu yetu kama wanahabari ni kupasha habari, kuelimisha na kuburudisha jamii kwa weledi wa hali ya juu. Pamoja na kuwapasha habari tunapaswa kuwa sauti ya wananchi,” amesema.
Nape amesema Serikali inafanya juhudi kubwa kufungua fursa mbalimbali zinazolenga kuboresha tasnia ya habari lakini bado kuna changamoto lukuki.
Miongoni mwa changamoto hizo ni bado tasnia ya habari kutokuwa na hadhi inayostahili hali inayosababisha wasio wanataaluma kuvamia.
“Bado hatujafanikiwa kuifanya tasnia ya habari kuwa taaluma yenye hadhi na heshima kama ilivyo kwa taaluma nyingine. Kuna kigugumizi hapa.
“Bado ujira na maslahi ya wanahabari yako chini na ya kusikitisha. Tupo katika mazingira ambayo wanahabari hawana mikataba, hawalipwi stahiki zao kwa wakati,” amesema.
Changamoto nyingine ni kuendelea kupungua kwa kasi kubwa ya habari za uchunguzi.