Waziri Kwandikwa afariki dunia akitibiwa Dar

Muktasari:
- Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Elias Kwandikwa amefariki dunia usiku huu akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam.
Mwanza. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Elias Kwandikwa amefariki dunia usiku Jumatatu Agosti 2, 2021 akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kufariki dunia kwa Kwandikwa ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ushetu Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, zimethibitishwa na Katibu wake wa masuala ya jimboni, Julius Lugobi.
"Ni kweli amefariki dunia na kwa sasa nipo kwenye pikipiki narudi Mjini Kahama nilikuwa huko vijijini lakini baada ya kutokea msiba imebidi nigeuze. Naomba unitafute baadaye maana nipo kwenye pikipiki kuna upepo mkali hatusikilizani vizuri" amesema Lugobi
Japo hakuelezea zaidi, taarifa zinaeleza Waziri huyo alikuwa amelazwa kwa matibabu katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kahama, Emmanuel Mbamange amesema kifo cha Waziri huyo ni pigo kwa wapigakura wake, Wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla na kuwaomba wana CCM na wananchi wote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu.
"Tumepoteza kiongozi jasiri na mahiri; Ushetu wamepoteza mbunge, Kahama, Shinyanga na Taifa limepoteza kiongozi mahiri. Tumeshtushwa sana na taarifa za kifo chake," amesema Mbamange
Ameongeza; "Natarajia kuitisha kikao cha Sekretarieti ya Wlaya ya CCM kujadili suala hili na baadaye Kamati ya Siasa kabla ya kutoa taarifa zaidi kuhusu msiba huu. Hakika ni pigo kubwa."
Kabla ya kuteuliwa katika nafasi yake ya sasa aliyokuwa akiitumikia, Kwandikwa amewahi kuhudumu katika nafasi ya Naibu Waziri wa Ujenzi Masilia na Uchukizi akiwa chini ya Isack Kamwelwe.