Waziri Kairuki akemea upigaji madai ya walimu

Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki
Dodoma. Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki, amewaonya viongozi wanaoomba fedha walimu ili washughulikie madai yao waache kufanya hivyo kwa kuwa hiyo ni rushwa na dhuluma.
Alisema viongozi hao hutoa sharti la kupewa sehemu ya fedha atakazopata mwalimu husika ili ayashughulikie madai hayo.
Onyo hilo amelitoa jana jijini hapa wakati akifungua mkutano wa maofisa utumishi wa halmashauri na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), ambapo alisema anapokea malalamiko mengi kutoka kwa walimu.
Alisema baadhi ya walimu pia humtumia ujumbe wa simu Rais, Samia Suluhu Hassan na kumuandikia barua kulalamikia kadhia hiyo.
“Kuna viongozi wanageuka kuwa miungu watu, wananyanyasa watumishi, wengine kuwatolea lugha zisizo na staha, kuwatukana na kuwatisha. Yaani mtu anadai haki yake halafu anawekewa mazingira ya kutoa rushwa. Vitendo kama hivi havikubaliki, atakayebainika tutaendelea kuchukulina hatua,” alisema Kairuki.
Alisema walimu wengi wanalalamikia kutopandishwa vyeo na mbaya zaidi, kuna walimu ili jina lake liingizwe kwenye orodha lazima atoe fedha.
Kairuki aliwataka watendaji hao kutimiza wajibu na waache kuwanyanyasa walimu. “Hakuna mtu aliyewalazimisha kufanya hii kazi walitaka wenyewe, kama hamuwezi kuwahudumia watumishi wenzenu muondoke.”
“Labda wengine wana madai ya likizo ama uhamisho wanaenda kwa kamisheni za asilimia kwamba unadai milioni kadhaa ili uweze kupata ni lazima utoe hela, jamani hivi vitu haviwezekani ndugu zangu ni lazima vifike mwisho,”alisema.
Kikosi kazi
Waziri Kairuki alisema wapo watumishi walioripoti kazini Juni mwaka huu, bado hawajalipwa stahiki zao, aliamuru maofisa utumishi kuhakikisha wanawalipa kwa wakati.
Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, Dk Charles Msonde alisema tayari hatua ya kuunda kikosi kazi cha kusikiliza kero za walimu kimeundwa na kitaanza kazi muda wowote kuanzia sasa.
Alizitaja changamoto hizo ni upandishaji wa madaraja, kupishana kwa muda wa kupandishwa madaraja hayo bila utaratibu na mfumo wa kubadilishwa vyeo cheo.
Naye Katibu Mtendaji wa TSC, Paulina Mkwama aliishukuru Serikali kwa kutoa vitendea kazi ikiwemo magari 16 na kompyuta 159 kwa watendaji wa tume hiyo.
Mwalimu na kiongozi wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Samson Mkyota alisema anaamini waziri amezungumza kupitia uzoefu alioupata.
Hivyo, aliwataka watumishi wa wa TSC kusoma hotuba za viongozi ambazo ni dira ya kuwaongoza kuwasaidia katika utumishi wao.