Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Aweso: Kuna upungufu lita milioni 10 za maji Mwanza

Muktasari:

  • Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema hitilafu iliyotokea katika mitambo ya kusukuma maji iliyoko Mabatini jijini Mwanza imechangia kuwepo kwa upungufu wa huduma ya maji jijini humo.


Mwanza. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema hitilafu iliyotokea katika mitambo ya kusukuma maji iliyoko Mabatini jijini Mwanza imechangia kuwepo kwa upungufu wa huduma ya maji jijini humo.

Pia, amesema mitambo ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoa wa Mwanza (Mwauwasa) ina uwezo wa kuzalisha lita milioni 90 za maji kwa siku huku akisema hitilafu hiyo imechangia upungufu wa lita milioni 10 na kufanya lita zinazozalishwa kwa siku kufikia milioni 80.

Aweso ametoa taarifa hiyo leo Ijumaa Julai 22, 2022 alipofanya ziara yenye lengo la kujua hali ya upatikanaji wa maji jijini Mwanza kutokana na maombi maalum yaliyowasilishwa Ofisini kwake na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula.

Ametaja maeneo ambayo yatapata upungufu wa huduma ya maji ni maeneo yenye miinuko hasa milimani huku akisema jitihada za kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kulingana na mahitaji zinaendelea kufanyika.

Pia, amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyere kuweka ratiba maalum ili kuhakikisha wakazi wa maeneo ya milimani wanapata maji kama ilivyo kwa wakazi wa maeneo mengine.

"Rais ameshatoa maelekezo mahsusi hataki kusikia, hataki kuona taharuki katika suala zima la maji, sisi kama viongozi tumefika, tumejionea na tumejipanga kuhakikisha hili jambo linafanyika haraka ili tuweze kurudi katika hali ya kawaida," amesema

Ameongeza,"wananchi katika jiji hili la Mwanza hasa katika maeneo ya miinuko tuwe watulivu katika kipindi hiki cha mpito lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha mitambo yetu inarekebishwa na inarudi katika hali yake ya kawaida na wana jiji la Mwanza wataendelea kupata huduma ya maji safi na salama."