Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazazi wanawapa wanafunzi dawa za kuzuia mimba

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wazazi wilayani Rungwe wamewaingiza watoto wao kwenye matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa siri ili kuwakinga wasipate mimba wakiwa wanaendelea na masomo, huku wauzaji wa maduka ya dawa wakihusishwa katika kutoa huduma hiyo.

Mbeya. Kutokana na fedheha na maneno mabaya katika jamii inayowazunguka watoto waliopata mimba wakiwa shuleni, wazazi wilayani  Rungwe mkoani Mbeya wamewaingiza watoto wao kwenye matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Wazazi wamechukua uamuzi huo baada ya kuwaona watoto wa chini ya miaka 18 wakipata mimba na wengine kuacha shule kwa sababu hiyo, kitendo ambacho kimekuwa kikiwafedhehesha katika jamii kwa kuonekana hawajui kulea.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hospitali ya wilaya ya Rungwe kwa miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba 2023, waliojifungua wakiwa na umri chini ya miaka 18 ni 349.

Mwananchi limefanya uchunguzi na kubaini kuwa wapo wazazi walioamua kuwaanzishia watoto wao matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa kuwapa vidonge, kuwachoma sindano, kuwawekea vijiti na wengine kutumia njia za kienyeji hadi pale watakapomaliza shule.

Asifiwe Mwakanosya amesema amechukua uamuzi huo baada ya kuona mwenendo wa mwanaye haupo sawa na amekuwa akimuonya mara kwa mara kuwa na makundi ambayo mienendo yao si mizuri.

“Nikiangalia mwanangu yupo kidato cha pili na hapo ndipo watoto wengi huku wanaharibikia kwa kupata mimba, nimeona bora nimpe dawa za kuzuia mimba kwani sihitaji zisizo na baba,” amesema Asifiwe.

Amesema ameona wazazi ambao watoto wao wamepata mimba wakiwa shule wanavyohangaika kulea watoto wenyewe kwani wengi wao wamekimbiwa na wanaume  na wengine ni waume za watu, hivyo wanakataa kutoa matunzo.

Alichofanya amemuwekea  mwanaye vijiti kupitia mtu wa duka la dawa kwa kutambua kuwa hospitali hawaruhusu watoto walio chini ya miaka 18 na wenye changamoto za kiafya, kutumia njia za uzazi wa mpango.

Atupele Galatoni amesema ana wasichana wawili wanaosoma kidato cha pili na tatu endapo watapata mimba hatokuwa na msaada kwa kuwa yeye ndiye mlezi wa familia, hivyo ameamua kutumia njia ya uzazi wa mpango kuwakinga na mimba.

“Nauza ndizi, nazunguka kwenye magulio mbalimbali ili kulea watoto wangu ambao hawana baba, leo hii mwanangu akija kuniletea mimba nitakuwa kwenye hali gani, ndiyo maana nimeamua kuwapa dawa za kuzuia mimba,” amesema.

Amesema kwa kuwa bado hawajafikisha miaka 18, anachokifanya ananunua vidonge yeye na kuwapa watoto wake na anahakikisha kila siku wanakunywa mbele yake.

Kwa upande wake, Gwamaka Mwaipopo amesema baada ya mtoto wake wa kwanza kupata mimba akiwa shule, walishauriana na dada yake njia ya kuwazuia watoto wengine wasipate.

“Kinga ni bora kuliko tiba, nimeharibu mmoja ila kwa wengine waliobaki hapana maana nina mabinti watatu na hawana mama, hivyo dada yangu aliniambia atawalinda hao wengine kuepuka aibu kama ya mtoto wa kwanza ambaye amenifanya nikose uhuru wa kuongea katika jamii,” amesema.

Amesema wazazi wengi wanaogopa kuripoti matukio ya ujauzito kwa sababu ya kulinda ujamaa, hivyo wanayamaliza kifamilia ili kuepukana na hilo hataki watoto wake wengine waangukie huko.

“Najua kabisa kuwafanyia kitu kitakachowazuia kupata mimba ni kama kuwaruhusu kufanya ujinga, lakini itapunguza kubeba mizigo ambayo haina ulazima katika familia ya kulea watoto wasiokuwa na baba, muhimu kuongea nao,” amesema Mwaipopo.

Watumiaji wa vidonge

Lusiana Mwakipesile, mwanafunzi ambaye amekuwa akipatiwa vidonge amesema mzazi wake alipoona marafiki zake wamepata mimba na kuacha shule, akajua na yeye atafanya hivyo.

“Rafiki zangu tuliokuwa tunasoma pamoja wote walipata mimba kidato cha pili kwa hiyo mama akajua kuwa na mimi nitakuwa mmoja wa hao, akaniambia niwe nakunywa dawa za kuzuia mimba.”

“Wakati mwingine huwa tunahadithiana kuhusu matumizi ya dawa hizi, wengine wamepelekwa kwa waganga wa kienyeji kupewa dawa na wengine wanachomwa sindano kwa siri kwa kuona kunywa dawa kila siku ni adhabu,” amesema.

Kwa upande wake, Grace Gabriel amesema amekuwa akipata  kizunguzungu cha mara kwa mara anapotumia vidonge vya uzazi wa mpango na kuelezwa kuwa ni kitu cha kawaida.

“Nikinywa vidonge naumwa kichwa, wakati mwingine najisikia kizunguzungu baada ya kumuelezea dada yangu aliniambia ni kawaida na alinibadilishia muda wa kunywa badala ya asubuhi ananipa usiku,” amesema Grace.

Akizungumza wa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe, Kitumbika Isaya amesema wazazi wengi wanaotumia njia hizo wanafanya kwa usiri na wanawatumia watu ambao hawana utaalamu wa masuala ya uzazi wa mpango.

“Sheria hairuhusu matumizi ya uzazi wa mpango kwa vijana, wazazi wanakwenda  katika maduka ya dawa, wanafanya vitu kwa siri lakini  baadaye wanakuja hapa kutafuta tiba  za athari ya njia walizotumia,” amesema Kitumbika.

Amesema wazazi kutumia njia hizo kwa watoto ni kuhalalisha kufanya ngono, hivyo njia salama ni kuzungumza na vijana wao waendelee kusubiri hadi wakati utakapofika.

Kitumbika amesema wanatumia kuwazuia mimba lakini wanasahau kama kuna magonjwa ya zinaa, hivyo anaepukana na mimba kwa kuhofia fedheha anakutana na matibabu ya magonjwa ya zinaa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Miriam Mgonja amesema njia zote zimefanyiwa utafiti na zinafanya kazi vizuri, hivyo ni mara chache moja wapo kufeli pia hawashauri mtu kutumia kwa siri bali kwenda hospitali kupata elimu, vipimo na ushauri.

Pia, amesema Wizara ya Afya imeanzisha kliniki rafiki za vijana ambapo kwa vijijini bado hazijafika, ikiwa na nia ya kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana kutokana na utandawazi.   

“Hawa vijana ndiyo kwanza wanaanza safari ya maisha wakianza hayo mambo hata ndoto zao zinaweza zikaishia njiani,   njia hizi inategemeana na mwili wa mtu katika kuhimili matumizi yake. Muhimu  kwenda sehemu husika na si kutumia njia za panya,” amesema Dk Miriam.