Wanafunzi wabainika vinara matumizi ya P2

Muktasari:
Kundi la wanafunzi na wanawake wametajwa kutumia kwa wingi njia za kisasa za uzazi wa mpango za vidonge vya dharura maarufu kwa jina la P2 na sindano kwakuwa njia hizo ni za siri ukilinganisha na nyingine.
Kasulu. Wanafunzi wa kike na wanawake wametajwa kutumia kwa wingi njia za kisasa za uzazi wa mpango za vidonge vya dharura maarufu kwa jina la P2 na sindano kwakuwa njia hizo ni za siri ukilinganisha na nyingine.
Pia wanawake walio kwenye ndoa, wilayani hapa mkoani Kigoma, wametajwa ni kundi linalotumia kwa wingi njia za kisasa za uzazi wa mpango za sindano na vidonge vya dharura.
Akizungumza na Mawananchi leo, Aprili 9,2021, Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Robert Rwebangira amesema kundi hilo limekuwa likitumia njia hizo kwasababu ni njia ya siri ambazo mtu mwingine hawezi kujua.
Amesema kwa mwaka 2020 zaidi ya wanawake 6,000 walitumia njia ya kisasa ya uzazi wa mpango ya sindano kwa kujificha kulingana na mazingira yanayowazunguka huku wanawake waliokwenye ndoa wanatumia njia hiyo ili waume zao wasijue.
Amesema wanawake 4,600 katika halmashauri hiyo walitumia njia ya uzazi wa mpango wa dharura ya vidonge kwa mwaka 2020 ambapo wengi wao ni wa miaka 15 hadi 19 huku vijana wa kiume wa umri huo wanatumia kondomu.
Amesema wanawake wamenatumia njia za muda mfupi za kisasa za uzazi wa mpango wakitumia sindano na vidonge bila ya ushauri wa wataalamu wa afya na matokeo yake wamepata madhara ya kiafya ikiwemo kuchelewa kubeba ujauzito pindi wanapokuwa tayari.
“Sindano ina vichocheo kama vya mwili na ikitumika kwa muda mrefu inaweza ikaingilia mfumo wa hedhi ya mwanamke na kushindwa kupata ujauzito itashusha mfumo wa uzazi wa kuchochea mayai kukua na kushindwa kupata ujauzito kwa muda mrefu,”amesema Rwebangira.
Amesema njia ya sindano ni ya muda mfupi ambayo mwanamke anaitumia akijitathimini kama anataka abebe ujauzito baada ya muda gani.
Mkazi wa mtaa wa Mwibuye, Winifrida John amesema wamekuwa wakitumia njia hizo kwa siri kwasababu waume wao wanataka waendelee kuzaa watoto wengi zaidi ilhali kipato chao ni kidogo kisichowezesha mahitaji ya familia.
“Mimi nimeona kwa wenzangu unakuta ana watoto sita hadi saba amezaa bila kufuata mpangilio halafu wanashindwa kuwatunza kwa kuwapa huduma muhimu hivyo mimi niliamua kwenda kufuata huduma ya uzazi wa mpango ya sindano kimya kimya,”amesema Farida Ibrahim.