Wazazi walaumiwa kuwaficha watoto wenye VVU Mtwara

Mshauri wa Mabadiliko ya Tabia na Mawasiliano wa Mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini, Edward Uisso akizungumza katika mafunzo ya wauguzi na viongozi wa Mkoa wa Mtwara. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

Imeelezwa kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafungia ndani watoto wenye maambukizi ya VVU/UKIMWI na kushindwa kuwapeleka katika vituo vya afya kwaajili ya kupata dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi ARV’S.

Mtwara. Baadhi ya wauguzi mkoani Mtwara wamewalaumu baadhi ya wazazi mkoani humo kwa kushindwa kuwapelekea watoto kupata dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi huku wakiwafungia ndani.

Akizungumza katika kikao kilichohudhuriwa na wauguzi na viongozi wa dini kupitia mradi wa USAID afya yangu Kanda ya Kusini, ofisa Muuguzi Mwandamizi wa Hospitali ya Mangaka Wilaya ya Nanyumbu, Janeth Chikawe amesema kuwa watoto wengi wanafungiwa ndani na kukosa haki zao za msingi.

Amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa watoto wanaofika katika vituo vya afya kupata dawa watoto kuanzia miaka 15 kushuku chini ambapo wamekuwa wakiwapa mafunzo na mifano mbalimbali ili kuwafanya wakumbuke kumeza dawa hizo.

“Unajua tatizo kubwa ni watoto chini ya miaka 5. unakuta mtoto anaishi kwa baba lakini kadi iko kwa mama mtoto anakosa haki yake kwa kuwa tunashindwa kumpima na tunashindwa kufuatilia maendeleo yake kiafya,” amesema Chikawe.

“Wapo wazazi wengi hawataki watoto wajue hali yao hii inatupa changamoto katika utoaji wa elimu ambapo tunapaswa kuwaelimisha mpaka afikie miaka 10,” amesema.

“Hapo ndipo tunamwambia ukweli lakini awali tunamwambia kuwa ana mdudu tu bila kujua shida yake na wengine tunawacholea askari akiwa na bunduki, ina maana tunamwambia kuwa kila mwili wa binadamu una ulinzi,” amesema.

"Wazazi wanawaficha watoto hawaweki wazi jambo hilo linatupa wakati mgumu lakini tukifanikiwa kutumia mfano wa askari wengi wanatambua na wanafika kupata elimu sahihi waishi vipi na maambukizi ya VVU/UKIMWI”

Naye Mchungaji wa Kanisa la TRMS Mei Likoyo alisema kuwa ili mtoto aweze kuishi na kufikia malengo yake wazazi hawanabudi kuwaambia ukweli na kuacha kuwafungia ndani.

“Natoa rai kwa wazazi wasifiche watoto wawapeleke kwenye vituo vya afya ili wapate dawa za ARV kitendo cha kuwaficha ni kuwakosesha haki yao ya msingi na kuona sio muhimu ama aibu hii ni kuangamiza taifa la kesho matibabu yao yapo kwanini wasipelekwe kwenye matibabu,” amesema Mchungaji Likoyo.