Wawili wajeruhiwa mlipuko lori la mafuta Mbeya

Baadhi ya askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji Mkoa wa Mbeya wakiwa eneo la tukio
Mbeya. Watu wawili wamejeruhiwa na kukimbizwa Hosptali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) kwaajili ya kupatiwa matibabu baada ya lori lililokuwa limehifadhiwa mafuta ya diseil kulipuka kutokana na kujaa gesi.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano, June 22, 2023 saa 4.45 asubuhi na kudaiwa kuwa ‘tanki’ hilo lilikuwa limekaa kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja katika kituo cha mafuta cha Infinity kilichopo eneo la Mafiati jijini hapa.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Meneja wa kituo hicho cha mafuta, Frederick Donard amesema kuwa sababu kubwa ya mlipuko huo ni kufuatia tenki hilo kujaa gesi kutokana na kukaa kwa muda mrefu juani.
“Hawa vijana waliojeruhiwa tumewakimbiza hosptali na afya zao zinaendelea vizuri, tukio limetokea walikuwa wakilifanyia marekebisho na kulisafisha na ndipo ukatokea mripuko uliotokana na gesi kujaa” amesema.
Amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Ally Mshana na Erick Samweli ambao wamepatiwa matibabu na hali zao ziko vizuri.
Naye Mratibu Msaidizi wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Gervas Fungamali amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanashukuru mlipuko haukuleta madhara makubwa.
Baadhi ya mashuhuda wamesema kuwa tukio hilo limezua taharuki kubwa kwa wananchi hususan wafanyabishara na kuomba Serikali kudhibiti magari yaliyohifadhiwa mafuta.