Chura asimulia ajali ya Noah, Fuso ikijeruhi wanane Mikumi

Gari aina ya Noah iliyopata ajali alfajiri ya leo Jumatano Juni 7,2023 katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kusababisha majeruhi.
Muktasari:
- Ajali ya gari iliyohusisha gari aina ya Noah pamoja na Fuso imetokea usiku wa kuamkia leo Hifadhi ya Mikumi na kusababisha majeruhi.
Morogoro. Ajali iliyohusisha gari aina ya Noah pamoja na Fuso imetokea usiku wa kuamkia leo Jumatano ya Juni 7, 2023 katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kusababisha majeruhi, huku ikiacha foleni kubwa ya magari.
Kwa mujibu wa dereva wa Fuso iliyopata ajali hiyo, Edward Chura amesema imetokea majira ya saa tisa usiku.
"Hii Noah ilikuwa inatoka mwelekeo wa Mikumi inakwenda Morogoro ikagonga gari iliyokuwa inapishana nayo (lori), ikayumba ikaja kukutana na gari yangu (Fuso) uso kwa uso," amesema.
Chura amesema kwenye Fuso aliyokuwa anaendesha ilikuwa inatoka Dar es Salaam kuelekea Iringa na hakuna majeruhi yeyote.
"Dereva wa Noah alikuwa anasinzia akagusana na lori akanifuata mimi ila kwenye gari yangu hakuna aliyejeruhiwa zaidi ya kuanguka na kutupwa nje ya barabara," amesema Chura.
Amesema magari yalikaa barabarani kwa muda mrefu na kusababisha foleni kubwa hadi Jeshi la Polisi lilipofika kuanza kutoa msaada wa kuwaondoa majeruhi na magari kuanza kupita saa 1 asubuhi.
Shuhuda mwingine ambaye hakutaja jina lake, amesema watu waliokuwa kwenye Noah wote wamejeruhiwa.
"Dereva kavunjika miguu, wengine wamevunjika mikono," amesema.
Mwananchi imefika Hospitali ya Mtakatifu Kizito Mikumi walipopelekwa majeruhi kujionea hali wanayoendelea nao.
Akizungumzia hilo kwa niaba ya Mganga Mkuu, Dk Steven Mbilinyi amesema wamepokea majeruhi nane wakiwa mahututi lakini wanaendelea na matibabu.
"Wote ni wanaume, hakuna aliyefariki ila wapo walioumia kichwani na waliovunjika miguu na mikono. Wote wanaendelea na matibabu ya awali. Tunafikiria wote kuwahudumia hapahapa," amesema Dk Mbilinyi.
Taarifa zilizoifikia Mwananchi kutoka kwa moja wa askari wa hifadhi hiyo ya Mikumi ambaye hakutaka kuandikwa kwani si msemaji, amesema ajali hiyo imetokea alfajiri na kwamba wao wameanza kusaidia majeruhi na kuwawahisha katika Hospitali ya St Kizito iliyopo Mikumi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alipopigiwa kuhusiana na ajali hiyo, amesema anafuatilia na taarifa itatolewa.
Aidha imeelezwa kuwa kutokana na ajali hiyo kumekuwa na foleni ndefu ya magari ndani ya Hifadhi hiyo ya Taifa ya Mikumi.
Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia mitandao yetu.