Dereva wa Coaster iliyoua watano, kujeruhi 20 Iyovi asakwa

Muktasari:
- Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito Mikumi, Dk Stephen Mbilinyi amethibitisha kupokea miili mitano ya marehemu na majeruhi 20, huku waliofariki wakiwa wanawake wawili na wanaume watatu.
Morogoro. Polisi mkoani Morogoro wanamtafuta dereva wa gari dogo aina ya Coaster ambaye jina lake halijafahamika, ambaye ametoroka baada ya kusababisha ajali iliyopelekea vifo vya watu watano na majeruhi 20 katika eneo la Iyovi Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema ajali hiyo imetokea leo Jumatano Juni 5,2023 na kuwaomba wananchi kutoa taarifa endapo watamuona huku akimtaka dereva huyo ambaye jina lake halijafahamika kujisalimisha.
Mkama amesema dereva wa Coaster alikuwa akijaribu kulipita kwenye kona lori lililokuwa mbele yake wote wakiwa katika mwelekeo mmoja ndipo alipokutana na lori la mafuta na kugongwa ubavu wa kushoto.
Amesema majeruhi tisa wamelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wakiendelea na matibabu huku majeruhi mmoja akihamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata.
Majeruhi katika ajali hiyo John Kameta mkazi wa Dar es Salaam ambaye alipandia Iringa, amesema anachokumbuka kabla ya ajali kutokea mbele yao kulikuwa na gari iliyoharibika ikiwa imebeba makaa ya mawe kutokana na dereva kuwa kwenye mwendo kasi akashindwa kujizuia akarudi kati ili aweze kupita jambo lililomshinda.
“Ile anarudi kati gari ya mafuta ikawa inapandisha ikajitahidi kuokoa maisha yetu, dereva akaingia porini ili sisi tunyooshe yule dereva wetu kwa kuwa mwendo wake ulikuwa mkali alishindwa kujiongeza akaifuata tena kwa hiyo ikapiga pembeni ndio tukapata matatizo haya,”amesema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito Mikumi, Dk Stephen Mbilinyi amesema wamepokea majeruhi 20 na miili mitano ya merehemu na kwamba katika watano ambao walikuwa wamefariki eneo la tukio wanawake walikuwa wawili na wanaume watatu wote wa umri wa kati.
Dk Mbilinyi amesema majeruhi tisa walihudumiwa kama wagonjwa wa nje kwa maana ya kuwa na mjeruhi madogo na kuruhusiwa, lakini majeruhi 11 walikuwa mahututi na miongoni mwao wamempa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kutokana na changamoto katika mfumo wa upumuaji wa viashiria vya damu kuvujia kwenye mapafu.
“Wagonjwa kumi wamelazwa katika hospitali yetu ambao wana chanagamoto tofauti wengine wamevunjika kwenye miguu wngine mikono na wengine majeraha kwenye kichwa lakini wote wanaendelea vizuri na matibabu yanaendelea,” amesema.