Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wawili wafariki dunia kwa kufukiwa na kifusi kwenye mgodi usio rasmi

Wachimbaji wadogo wakiwa eneo la magenge wilayani Geita kulikotokea ajali ya wachimbaji wadogo kufukiwa na kifusi

Muktasari:

  • Waliofariki ni Rashidi Twangake (33) mkazi Nyakayondwa Chato aliyekuwa fundi na Masunga Nyangota mkazi wa Bariadi aliyekua mchimbaji mdogo.

Geita. Wachimbaji wawili (maarufu Manyani) wamepoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba dhahabu kwenye machimbo yasiyo rasmi yaliyopo Magenge wilayani Geita mkoani hapa.

Mkaguzi Msaidizi kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, Wambura Fidel amesema vifo hivyo  vimetokea Juni 5,2024 baada ya wachimbaji hao kuingia kwenye eneo lenye leseni ya utafiti na kuchimba kinyemela.

Amesema wakati wakiendelea na uchimbaji ndipo walifukiwa na kifusi na shughuli za kutoa miili hiyo zimefanywa na wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na Jeshi la zimamoto.

Waliofariki ni Rashidi Twangake (33) mkazi Nyakayondwa Chato aliyekuwa fundi na Masunga Nyangota mkazi wa Bariadi aliyekua mchimbaji mdogo.

Kevin Samweli ambaye ni mchimbaji mdogo amesema ajali hiyo imetokana na ufungaji matimba hafifu uliosababisha shimo lisiwe imara na kusababisha udongo kuporomoka.

“Ajali hii imesababishwa na ufungaji matimba hafifu watu wanafanya kinyemela hawana mwongozo mtu anatoka nyumbani na anakuja kutafutia familia kwa kujificha na ndio matokeo yake  haya.”

“Sisi vijana tunalazimisha kitu hata kama unaona hakiwezekani saa nyingine ni shida ya kutafuta pesa ndio inachangia yote haya,”amesema  Samwel.

Amesema mashimo katika eneo hilo yapo tangu 2013 na wachimbaji wadogo maarufu manyani huingia kinyemela kutafuta riziki na kuwa hilo sio tukio la kwanza, kwani miaka ya nyuma walifukiwa wachimbaji wengine na eneo kufungwa lakini bado wachache huingia kinyemela.

Diwani wa Kata ya Magenge, Edwad Msungwi amesema ajali hiyo imetokana na uchimbaji usio rasmi uliosababisha nguvu kazi ya Taifa na kuiomba Wizara ya Madini kuwabana wenye leseni ili wasimamie maeneo yao kuzuia uchimbaji holela.

Aprili 26 katika kata ya Nyarugusu Wilayani Geita mchimbaji mdogo Bahati Ngalaba alipoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi wakati akifanya ukarabati kwenye shimo.

Matukio ya wachimbaji wadogo kufukiwa na kifusi hutokea mara kwa mara ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2023 wachimbaji wadogo 13 waliripotiwa kupoteza maisha mkoani hapa,  wakiwa kwenye shughuli zao za uchimbaji na 10 kati yao waliingia kinyemela kwenye maeneo yasio rasmi.