Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waungeni mkono wanawake kuleta usawa wa kijinsia – Mdeme

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, anayeshughulikia Maendeleo ya Wanawake, Felister Mdeme. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Wapo baadhi ya wanaume wanaogopa wanawake kufanikiwa wakiamini hilo likitokea watawanyanyasa.

Tarime. Wanaume nchini wametakiwa kuwaunga mkono wanawake katika harakati za kuleta usawa wa kijinsia.

Imeelezwa kuwa suala la usawa wa kijinsia haliwezi kuondoa ukweli kuwa daima mwanamke atabakia kuwa mwanamke na mwanamume atabakia kuwa mwanamume katika mgawanyo wa majukumu kwa usawa wa kijinsia.

Haya yamesemwa leo Jumapili Aprili 13,2025 mjini Tarime na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, anayeshughulikia Maendeleo ya Wanawake, Felister Mdeme  wakati wa akizindua kampeni ya ‘Amsha ari’.

Kampeni hiyo ina lengo la kuleta mageuzi ya kifikra na mtazamo ili kuwafanya wananchi kujua umuhimu wa kushiriki katika maendeleo.

Mdeme amesema suala la usawa wa kijinsia linalenga kuunganisha jamii na kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo endelevu kwa masilahi ya Watanzania wote.

Amesema wapo baadhi ya wanaume wanaogopa kuunga mkono harakati hizo wakidhani endapo kutakuwa na mafanikio katika suala hilo, watanyanyaswa na wanawake jambo ambalo sio kweli.

"Hii hamsini kwa hamsini haina maana ya kuwa mwanamke ataacha majukumu yake  yale ya  asili, hapana ataendelea  kuwa mwanamke, mke, mama na mlezi wa familia," amesema Mdeme na kuongeza;

"Sio kweli kuwa tukifanikiwa katika hii hamsini kwa hamsini kwamba mambo yatabadilika kule nyumbani eti mama akifika atamtaka baba aingie jikoni kupika au kuosha vyombo, hapana, mama ataendelea kuwa mama na baba ataendelea kuwa baba vile vile."

Naibu katibu mkuu huyo amesema harakati za kuleta usawa wa kijinsia katika jamii haziwezi kufanikiwa endapo wanaume hawataziunga mkono jitihada hizo huku akisisitiza ili kupata mafanikio, wanawake wanawategemea wanaume katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya kijamii.

Akizindua kampeni hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amesema kampeni hiyo itakayofanyika nchi nzima, inalenga kuwezesha wananchi kubadili fikra na washiriki katika kujiletea maendeleo kwa ustawi wa jamii.

Amesema Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kusogeza na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kuanzia ngazi ya chini.

Mpanju amesema hata hivyo kwa namna moja ama nyingine, fursa hizo bado hazijatumiwa vema na wananchi katika kujiletea  maendeleo kutokana na dhana iliyojengeka kwa wananchi kuwa Serikali ndiyo inayowajibika kuwaletea maendeleo.

"Ipo haja ya kutengengeza mazingira wezeshi na shirikishi ili jamii iweze kushiriki kuanzia ngazi ya vitongoji, na ushiriki huu utasaidia kuwa na maendeleo endelevu, shirikishi na wezeshi hatua ambayo pia itasadia wananchi kuwa na uwezo wa kusimamia na kufuatilia huduma zote za msingi zinazotolewa kuanzia ngazi za chini," amesema Mpanju.

Amesema timu ya wataalamu kutoka wizarani kwa kushirikiana na wenzao kutoka wizara ya Katiba na Sheria, watafanya kazi ya kuelimisha jamii juu ya namna ya kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo itakayofanyika katika  kata zote 34 za Wilaya ya Tarime kwa siku 10 kabla ya kuhamia maeneo mengine nchini.

Amefafanua kuwa jamii itapewa ujuzi namna ya kushirikiana pamoja na kubuni, kupanga, kusimamia na kufuatulia miradi ya maendeleo kulingana na fursa zilizopo katika maeneo yao.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tarime akiwamo Annabeli Gikaro, wamesema kampeni hiyo imekuja muda muafaka na wananchi wanapaswa kuielewa vema ili kuyaishi yalipo katika kampeni hiyo.