Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watumishi saba wa Jiji la Arusha wahojiwa Takukuru

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo.

Muktasari:

  • Uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, unaendelea.

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, imesema imewahoji watumishi saba wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, kufuatia tuhuma za kughushi nyaraka, uchepushaji wa makusanyo ya Serikali na ubadhirifu wa fedha za umma.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Mei 22, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema miongoni mwa watumishi ni wa kitengo kinachohusiana na ukusanyaji wa mapato.

“Tunaendelea kuwahoji na wengine pia, tunakusanya nyaraka kwa ajili ya kutambua nini kimetokea na watakaothibitika kushiriki watafikishwa mahakamani,” amesema Ngailo.

Amesema bado wataendelea kuwahoji watumishi wengine sambamba na kuperuzi nyaraka mbalimbali kwa lengo la kubaini kilichotokea na wataangalia kwenye mfumo. “Kwa sababu  suala hili linahusu matumizi ya mfumo, tukikamilisha uchunguzi tutatoa taarifa,” amesema ofisa huyo.

Suala la ubadhirifu liliibuliwa mwishoni mwa wiki katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na wadau wa utalii, kilicholenga kusikiliza na kutatua changamoto zilizoko katika sekta hiyo.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini, alisema utekelezaji wa maelekezo aliyopewa na Makonda katika kikao cha kwanza cha Aprili 13, mwaka huu ndicho kilichomfanya akutane na wadau ili kubaini changamoto zao.

Hata hivyo, Makonda alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Mussa awasimamishe kazi watumishi hao kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi.

Katika kikao cha awali, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo aliibua tuhuma za kutozwa ushuru wa huduma Sh24 milioni, lakini risiti aliyopewa iliandikwa Sh3.6 milioni.

Miongoni mwa tuhuma zilizoibuliwa na Chambulo ni utengenezaji wa nyaraka bandia na kuchepusha baadhi ya makusanyo ya kodi, jambo lililomlazimu Makonda kuagiza uchunguzi wa Takukuru ufanyike.


Kikao cha awali

Katika kikao cha awali, Chambulo alionesha nyaraka alizodai zinathibitisha matendo maovu ya watendaji wa jiji hilo.

Katika ukurasa wa kwanza wa fomu aliyopewa na halmashauri hiyo, Chambulo alisema imeandikwa jina la kampuni yake, lakini namba za biashara na utambulisho sio zake.

Alidai kuwa watumishi hao walimpa namba ya malipo kwa ajili ya kulipia ushuru wa biashara wa Sh19 milioni ambao ni asilimia 0.3 ya pato ghafi.

Alielezea kushangazwa na fomu aliyopewa na halmashauri kuwa na taarifa tofauti na halisi aliyoijaza na kuikabidhi kwao.

“Hii nyaraka siyo ya kwangu, nyaraka niliyojaza ni hii hapa, alipata wapi jina linaitwa The Tanganyika Wilderness Camps, ukifungua hapa kwenye nyaraka ya halmashauri hii hapa(anaonyesha).”

“UKiangalia vizuri namba ya mlipaji hii siyo hata namba ya kwetu, hata tarakimu za simu imepungua moja kwa hiyo imebandikwa, yangu hii hapa (akionyesha fomu hizo),” alisema Chambulo.

Alisema hata utambulisho wa biashara inayoonekana katika fomu hiyo imejazwa tofauti na ya kampuni yake.

Katika kikao cha kwanza cha Aprili, Makonda aliagiza wakutane na wadau wa utalii na endapo watagundua kuna changamoto ya mkanganyiko wa kisheria kama liko kwenye mamlaka ya mkoa, wataliamua na kama linahitaji maelekezo kutoka wizarani lipelekwe huko.