Vigogo serikalini watajwa kikwazo vita dhidi ya rushwa nchini

Muktasari:
Utafiti wa ‘Afrobarometer’ umeonyesha kuwa asilimia 77 ya Watanzania wanaona kiwango cha rushwa kimepungua nchini, huku baadhi ya watendaji na watumishi, taasisi na vyombo ya Serikali wakiendelea kuwa kikwazo katika vita dhidi ya rushwa.
Dar es Salaam. Utafiti wa ‘Afrobarometer’ umeonyesha kuwa asilimia 77 ya Watanzania wanaona kiwango cha rushwa kimepungua nchini, huku baadhi ya watendaji na watumishi, taasisi na vyombo vya Serikali wakiendelea kuwa kikwazo katika vita dhidi ya rushwa.
Asilimia 84 ya wananchi wamesema Serikali inafanya jitihada za kutosha katika mapambano dhidi ya rushwa, hatua inayosababisha kupungua kwake.
Utafiti huo uliofanywa mwanzoni mwa mwaka jana na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa) ulilenga kuangalia mtazamo wa wananchi kuhusu hali ya rushwa nchini ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2017 ambapo asilimia 71 ya wananchi walisema rushwa inapungua.
Katika utafiti huo imebainika licha ya vitendo vya rushwa kupungua kwa kiasi kikubwa katika taasisi za Serikali, ikiwemo Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mahakama, bado kuna watumishi wanaoendeleza vitendo hivyo.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa asilimia 23 ya Watanzania wanaamini kwamba watumishi wote wa Jeshi la Polisi wanajihusisha na vitendo vya rushwa, huku asilimia 41 wakisema baadhi ya askari ndio wanafanya vitendo hivyo.
Akiwasilisha ripoti hiyo, mtafiti Thadeus Mboghina alisema wahojiwa wengi walionyesha kuridhishwa na juhudi za Serikali katika kukabiliana na rushwa, hali inayowaondolea mzigo wananchi wanaofuata huduma kwenye taasisi hizo za umma.
Alisema pamoja na mafanikio hayo, utafiti umeonyesha asilimia 62 ya wahojiwa wamekiri kuhofia au kuwafahamu wanaohofia kutoa taarifa za viashiria vya rushwa kwa kuhofia usalama wao.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi msaidizi wa udhibiti katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Omary Mzee alisema imeonyesha kuna mwendelezo mzuri katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Alisema Tanzania inakwenda kwa kasi kwenye mapambano dhidi ya rushwa, kutokana na utashi wa kisiasa wa viongozi wa juu wa kitaifa.
Alisema Takukuru inafanya kazi kubwa kuimarisha mifumo ya uchunguzi pamoja na kutoa elimu kwa umma, hatua zinazochangia kupungua kwa vitendo vya rushwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema utafiti wa Afrobarometer unafanyika katika nchi 35 za Afrika, ambapo wananchi wanapata fursa ya kueleza mitazamo yao kuhusu nyanja mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya mtendaji mkuu wa mahakama, Mkurugenzi wa mipango wa mahakama, Erasmus Uwiso alisema ripoti hiyo inaonyesha mafanikio katika juhudi za kupambana na rushwa kwenye mhimili huo.
‘‘Tunafurahi kuona juhudi kubwa zinazofanywa na mahakama katika kuongeza uwazi na uwajibikaji zinafanya kazi, ikiwemo kupambana na dalili zozote zinazoashiria rushwa. Tumeweka mfumo ambao unamuelekeza mwananchi kufuata hatua ili kupata huduma za kimahakama kuepusha vishoka kuingilia kati,’’ alisema.