Watuhumiwa wa wizi wa shehena ya mafuta waendelea kusota rumande

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro watuhumiwa hao wanaoendelea kusota rumande ni dereva wa lori la mafuta la kampuni ya Meru Abubakar Mwichangwe, pamoja na mameneja watatu wa vituo vya mafuta vya kampuni ya Simba Oil ambao ni Hamidu Sudi (50) mkazi wa Dar es Salaam, Abiner Shalon (25) mkazi wa Morogoro na Abdalah Nihed (30) mkazi wa Morogoro.
Morogoro. Watuhumiwa wanne wa wizi wa mafuta aina ya diesel yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wameendelea kusonda rumande bila ya kufikishwa mahakamani, huku Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro likidai kuwa uchunguzi bado haujakamilika.
Watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro ni dereva wa lori la mafuta la kampuni ya Meru Abubakar Mwichangwe, pamoja na mameneja watatu wa vituo vya mafuta vya Kampuni ya Simba Oil ambao ni Hamidu Sudi (50) mkazi wa Dar es Salaam, Abiner Shalon (25) mkazi wa Morogoro na Abdalah Nihed (30) mkazi wa Morogoro.
Akizungumzia hatua hiyo ya kuendelea kushikiliwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema kuwa uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo bado haujakamilika kwa kuwa uchunguzi huo polisi wanafanya kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
"Suala la mafuta hasa yale yanayosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine linahusika na mamlaka zaidi ya moja, hivyo kwenye huu wizi ambao kwetu sisi ni kosa la jinai lazima tushirikiane na hizo mamlaka nyingine ambazo ni TRA na Ewura katika kuchunguza tukio zima kabla ya kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, hata hivyo mara baada ya uchunguzi huu kukamilika basi tutawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria," amesema Kamanda Mkama.
Awali, Kamanda Mkama kwenye taarifa yake aliyoitoa Machi 17,2025 alisema Machi 16, 2025 mwaka huu dereva wa lori hilo la kampuni ya Meru pamoja na wenzake watatu ambao ni mameneja wa vituo vya mafuta vya Simba Oil walikula njama na kuiba mafuta aina ya diesel lita 35,700 yenye thamani ya Sh77.1 milioni.
Kamanda Mkama amesema mafuta hayo yalikwenda kumiminwa kwenye kisima cha kampuni ya Simba Oil Mkambarani Barabara ya Morogoro - Dar es Salaam na kingine kilichopo mjini Morogoro, baadaye dereva alikwenda kuliangusha kusudi lori hilo eneo na Iyovi kisha kulichoma moto kwa lengo la kupoteza ushahidi ama kuaminisha umma kuwa ni ajali kama zilivyo ajali nyingine.
"Dereva huyo alikuwa akiendesha lori hilo lenye shehena ya mafuta namba T. 661BXR/ T. 489 BHC aina ya FAO kampuni ya Meru akitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Lubumbashi nchini DR Congo," amesema kamanda Mkama.
Wakati polisi wakiendelea kuwashikilia watuhumiwa hao bado vituo vya mafuta vya Simba Oil vimeendelea kufungwa ambapo mmoja wa wanafamilia wa wamiliki wa kampuni hiyo, Arif Mbaraka amekiri vituo hivyo kufungwa kwa zaidi ya siku kumi sasa na hivyo kufanya kampuni hiyo kupata hasara ambayo bado hafahamu ni kiasi gani cha fedha.
Akizungumzia hasara waliyoipata kama kampuni baada ya vituo viwili kufungwa Mbaraka amesema ni hasara kubwa kwa kuwa yapo makampuni mbalimbali ya minara ya simu ambayo yameingia mkataba na kampuni hiyo wa kuchukua mafuta kwenye vituo hivyo.
"Kuna kampuni za minara ya simu ambazo zinachukua mafuta hadi lita 2000 kwa wiki kwa ajili ya kupeleka kwenye minara wateja hao wote tumeshawapoteza kwa muda huu ambao tumefungiwa lakini pia tukio hili limechafua jina la kampeni yetu," amesema Mbaraka.