Watuhumiwa kesi ya mauaji waachiwa huru

Muktasari:
- Hakimu Mkazi Mary Mrio amewaachia huru Bakari Tindwa na Richard Lulale, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji, kwa kile alichokisema upande wa mashtaka hawana nia ya kuendelea na shtaka hilo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru Bakari Tindwa na Richard Lulale waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji, baada Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuweka wazi nia ya kutoendelea na shauri hilo.
Inadaiwa kuwa kati ya Mei 16 hadi 19, 2023 maeneo ya jijini Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kumuua kwa makusudi Fatuma Bakari.
Washtakiwa hao wameachiwa huru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio leo Desemba 8, 2023 baada ya Wakili wa Serikali, Neema Moshi kuieleza Mahakama hiyo kuwa DPP ameliondoa shauri hilo chini ya kifungu namba 91(1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Hakimu Mrio amesema kutokana na hati hiyo iliyowasilishwa chini ya kifungu hicho, Mahakama hiyo inawachia huru washtakiwa hao kwa sababu upande wa mashtaka hawana nia ya kuendelea na shtaka linalowakabili.
“DPP amewaondolea shtaka kwa kifungu cha 91(1), mmeachiwa huru, hata hivyo haizuii kuwafungulia kesi kwa shtaka hilo hilo,”amesema Mrio.
Awali, kabla ya kuwafutia kesi hiyo, Wakili Moshi ameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya kutajwa, lakini DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo mahakamani hapo.
Baada ya washtakiwa hao kuachiwa huru wamepelekwa mahabusu kwa hatua nyingine.