Aachiwa huru baada ya kusamehewa na ‘mwanaye’

Muktasari:
- Mkazi wa Kiwalani Rajabu Mbwana (63) ameachiwa huru na Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo baada ya mdai Musa Majujume kuomba kesi hiyo iondolewe mahakamani kwa sababu mshtakiwa ni baba yake.
Dar es Salaam. Mkazi wa Kiwalani, Rajabu Mbwana (63) aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la shambulio la kudhuru mwili, ameachiwa huru na Mahakama ya Mwanzo Kariakoo baada ya mdai Mussa Majujume (35) kuomba kuiondoa kesi hiyo mahakamani.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Mei 3, 2023 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Claudis Kipande wakati mshtakiwa huyo alipokuwa anasomewa kwa mara ya kwanza shtaka analokabiliwa nalo.
Akisoma hati ya mashtaka, Karani Emmy Mwansasu ameiambia mahakama kuwa Mei Mosi 2023 saa 2:30 maeneo ya Ocean Road ndani ya Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, mtuhumiwa alimshambulia Majujume kwa kumchoma na mkasi upande wa kushoto ubavuni na mkononi kitendo ambacho ni kosa na kinyume cha sheria.
Mshitakiwa alipoulizwa na hakimu kuhusu tuhuma hiyo ya shambulio la kudhuru mwili alikana kuhusika.
Mshtakiwa huyo baada ya kukana kosa linalomkabili ndipo mdai Majujume alinyoosha mkono na kuieleza mahakama hiyo anaomba aiondoe kesi hiyo kwa sababu Mbwana ni baba yake hivyo amemsamehe.
Baada ya maelezo hayo hakimu Kipande alikubali ombi la mdai na kumwachilia huru mshitakiwa chini ya kifungu Cha 23 (a) cha nyongeza ya 3 ya MCA sura ya 11 toleo la mwaka 2019.