Dk Mpango atoa ujumbe wa Pasaka, Uchaguzi Mkuu

Dodoma. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi hususan wakinamama kuwaongoza watoto wao hasa vijana, kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Dk Mpango ametoa rai hiyo baada ya kushiriki ibada ya Sikukuu ya Pasaka leo Jumapili, Aprili 20, 2025 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais imesema, Dk Mpango amewasihi Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu kwa kuwa vurugu sio sehemu ya jadi ya Watanzania.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi wa kumchagua Rais, wabunge na madiwani, niwaombe sanasana wananchi tukashiriki uchaguzi, vurugu si sehemu ya jadi ya Mtanzania,” amesema Dk Mpango.
“Kwa wote watakaopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi tunawasihi sana wakazingatie sheria na miongozo waliyopewa, wakatende haki kwa wote watakaojitokeza kugombea uchaguzi.”
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na busara na umakini katika matumizi ya vyombo hivyo, ili kuepusha kupoteza maisha ya watu barabarani.

Makamu wa Rais amewatakia heri na baraka Watanzania wote katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka na kuwasihi kusherehekea kwa amani na furaha.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwenza wa Makamu wa Rais, Mama Mbonimpaye Mpango imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari.