Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watu wanne wadaiwa kubaka kisha kukimbilia bwawani

Wakazi wa Musoma wakiwa kwenye  bwawa la kitaji wakishuhudia  juhudi za kuwatoa watu wanne wanaodaiwa  kujificha ndani ya bwawa hilob aada ya kutuhumiwa kubaka na kujeruhi. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Juhudi za kuwatoa kwenye maji watu wanne wanaodaiwa kuhusika na tukio la ubakaji na kujeruhi lililoteka katika Mtaa wa Serengeti Manispaa ya Musoma zimegonga mwamba baada ya kutafutwa siku nzima ya jana bila mafanikio.

Musoma. Juhudi za kuwapata watu wanne wanaodaiwa kumbaka na kumjeruhi mama mmoja mkazi wa Manispaa ya Musoma zimegonga mwamba baada ya watu hao kukimbilia kwenye bwawa la Kitaji lililopo Musoma kwa lengo la kujificha.

Watu hao wanaodaiwa kukimbilia bwawani humo jana Juni 19, 2023 kwa lengo la kujificha walitafutwa siku nzima na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji bila mafanikio.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumanne Juni 20, 2023, Kamanda wa jeshi hilo mkoani Mara, Agostino Magere amesema hadi wanaondoka katika eneo la tukio jana saa 1.40 usiku hakuna mtu yeyote aliyepatikana katika bwawa hilo.

“Jana changamoto kubwa ilikuwa ni mazingira ya bwawa kwa ujumla kuna matope, magugu na kina kirefu nyasi zimeota kiasi kwamba inakuwa ni vigumu kuingia mle ndani,”amesema 

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Kelvin Onyango amesema vijana sita wanadaiwa kumbaka mwanamke mmoja asubuhi na kisha kukimbilia kwenye bwawa hilo baada ya kukimbizwa na wananchi.

“Walikuwa watu kama sita hivi wawili wakaelekea upande wa kule wanne baada ya kuona wamezingirwa wakaingia humu bwawani sasa tangu wameingia hawajatoka,”amesema 

Mwita Wambura amesema kuwa kazi ya kuwatoa watuhumiwa hao kwenye bwawa hilo ilikuwa ngumu kutokana na mazingira  ya bwawa hilo ambalo limefunikwa na magugu.

“Hapa kuna magugu maji yamefunika bwawa zima lakini pia chini kuna tope sasa inakuwa ni vigumu kuingia majini,kwahiyo hawa wazamiaji wanashindwa,” amesema 

Akisimulia tukio la ubakaji lilivyotokea, Majura Johnson amesema asubuhi akiwa anaelekea kazini alisikia sauti ya mama ikilia kuomba msaada kutokea kwenye jumba bovu liliopo pembezoni mwa barabara ya Serengeti Manispaa ya Musoma.

Amesema alipofika kwenye eneo hilo aliwakuta vijana sita mmoja akiwa uchi wa mnyama wakimbaka mama huyo na baada ya kumuona walikurupuka na kuanza kukimbia.

“Huyo mama alivuliwa nguo na kuchomwa na visu sehemu mbalimbali ya mwili wake lakini pia wakati wanakimbia wameondoka na mkoba wake,”amesema 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk Osmund Dyegura amethibitisha mama huyo kupokelea hospitalini hapo akiwa na majeraha ya kuchomwa na vitu vyenye ncha kali.