Watu 16 waokolewa ajali ya mabasi Same

Moshi. Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema watu 16 wameokolewa katika ajali iliyotokea wilayani Same ikihusisha basi kubwa na dogo, ambayo yaliwaka moto .
Amesema ajali hiyo iliyotokea leo Jumamosi Juni 28, 2025 imehusisha basi la abiria la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda mkoani Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same kwenda Moshi.

"Tupo njiani kuelekea eneo la tukio, lakini taarifa za awali ni kwamba basi la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kuelekea mkoani Tanga na Coaster iliyokuwa inatoka Same kuja Moshi Mjini yamegongana na kuwaka moto," amesema alipozungumza na Mwananchi.

Amesema juhudi za kuondoa miili na majeruhi zinaendelea eneo la tukio na waliookolewa ni 16.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amesema ajali hiyo imetokea jioni ya leo Juni 28.

"Kumetokea ajali mbaya, gari dogo la abiria na basi kubwa yamegongana uso kwa uso na kusababisha kuwaka moto, watu wameshindwa kutoka ndani ya hayo magari," amesema.