Watozwa faini ya Sh61 milioni kwa kuuza kemikali bei juu

Muktasari:
- Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewapiga faini ya Sh61 milioni wasambazaji saba wa kemikali aina ya Sodium Cyanide kwa makosa ya kuuza kemikali hiyo bei juu kinyume na bei elekezi iliyotolewa na serikali huku wengine wakibainika kuuza kwa watu ambao hawajasajiliwa.
Geita. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewatoza faini ya Sh61milioni wasambazaji saba wa kemikali aina ya Cyanide kwa makosa ya kuuza kemikali hiyo kinyume na bei elekezi iliyotolewana serikali huku wengine wakibainika kuuza kwa watu ambao hawajasajiliwa.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Januari 19, 2023 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo akizungumza kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, amesema wasambazaji hao wamebainika baada ya kikao cha Januari saba kilichotaka wasambazaji wasio waaminifu wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua.
Amesema mbali na wasambazaji kuuza kwa bei ya juu kinyume na maelekezo ya Serikali, pia wamebaini wasambazaji wanauza kwa masharti kwakuwalazimisha wale wanaotaka bei elekezi ya Sh600,000 kununua na bidhaa nyingine kama Carbon kinyume cha utaratibu na wale wanaopinga wanauziwa kwa Sh900,000 hadi Sh1.2 milioni.
Amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Madini iliunda timu maalumu ambayo ilitembelea mikoa ya Geita, Mwanza, Mara na Shinyanga na kubaini uwepo wa mapipa 4,423 sawa na tani 221.15.
Amesema kuanzia Desemba 2, 2023 hadi Januari 16, 2023 tani 1,062 zimeingia sokoni na kudhihirisha kuwa hakuna uhaba wa kemikali ya Sodium Cyanide nchini.
Pia, timu iliyoundwa ilibaini uwepo wa watumiaji wengi wa kemikali ambao hawajasajiliwa jambo ambalo ni kinyume na sheria hivyo kusababisha mamlaka kutotambua kiasi kilichoingia na jinsi kilivyotumika.
“Cyanide pamoja nakutumika kwenye uchenjuaji wa dhahabu bado ni kemikali hatari kwa viumbe, lakini ikichepushwa ni bashilifu inayoweza kutengeneza silaha ya maangamizi hii ni kemikali ambayo inatakiwa ifanyiwe usimamizi wa kutosha na anayetumia lazima ajulikane kwa mamlaka na hadi tumizi la mwisho linapaswa kujulikana,” amesema.
Aidha amewataka wasambazaji kutokwenda kinyume na sheria kwa kuwauzia watu ambao hawajasajiliwa sanjari na kuwataka kutii agizo la serikali la kuuza pipa lenye kilo 50 kwa Sh 600,000.
Katika kudhibiti utoroshaji wa kemikali hiyo Mamlaka ya maabara ya mkemia Mkuu wa Serikali imeweka utaratibu shehena ya Sodium Cyanide itakayoingizwa nchini kwa lengo la kuuzwa au kusambazwa itakuwa inafungwa latiri na wakaguzi wa mamlaka inapotoka bandarini na kufunguliwa na wakaguzi kwenye eneo la mwisho la mzigo unakofikia.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amewataka wasambazaji wajanja wajanja wanaofanya bei ya kemikali ya Sodium Cyanide ipande hawatafumbiwa macho na kuwataka kuuza kwa bei elekezi kwa kuwa mkono wa serikali upo pande zote.