MAWAIDHA: Mafunzo mema kupitia kisa cha Nabii Adam

Qur’an Tukufu imetaja maadili kupitia visa vya Mitume na Manabii, vinavyomhamasisha msikilizaji, na kumjengea imani thabiti itakayomwongoza katika safari yake ya kumtii Allah.
Katika safu hii, nitataja kisa cha Nabii Adam (rehema na amani ziwe juu yake), ambacho kimejaa maadili ya kimaisha yanayohitaji kutumika na kila mtu ili kuboresha tabia zake.
Kutaja maadili kabla ya kuumbwa binadamu
Kisa cha Nabii Adam kimetaja maadili hata kabla ya uumbaji wa binadamu mwenyewe, ikionyesha athari za ufisadi wa maadili. Allah Mtukufu anasema: "Na aliposema Mola wako kwa Malaika: 'Nitamuumba mtu mkaaji duniani.' Wakasema: 'Je, utaumba huko atakayefanya uharibifu na kumwaga damu…' (2:30). Kadhalika, kisa cha Nabii Adam kinahimiza kufuata amri za Allah na kujiepusha na makatazo, na kuelezea athari za kutotii. "Na wala msikaribie mti huu, mkawa miongoni mwa wakosaji." (2:35)
Sababu za upotofu wa maadili
Aidha, kisa cha Nabii Adam kinaelezea sababu za upotofu wa maadili, ambazo zinaweza kuwa sababu za nje, kama vile shinikizo la shetani na marafiki wabaya, au za ndani, kama vile kuikumbatia dunia na kushindwa kupingana na matamanio ya nafsi. "Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizofichiwa, na akasema: 'Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanaoishi milele.'" (7:20)
Uchaji Allah na athari za tabia mbaya
Kisa cha Nabii Adam kinahimiza kumcha Allah na kinatufundisha madhara ya dhambi kwa nafsi. Hili limeelezwa wazi na Qur’an. "Basi akawadanganya kwa hadaa. Walipokula ule mti (ulioharamishwa), tupu zao zilifichuka na walijifunika kwa majani ya Bustanini…" (7:22).
Kadhalika, kisa cha Nabii Adam kinatufundisha athari za ufisadi wa maadili kwa jamii, na kwamba si vyema kudharau madhara ya maadili mabaya kama vile udhalimu, wivu, na ubahili.
Hii inaonyeshwa kupitia kisa cha wana wa Adam, Kabil na Habil. "Na waambie habari za wana wa Adam kwa haki, walipoleta sadaka, moja ikakubaliwa, na nyingine haikukubaliwa. Akasema (mmoja kumwambia mwenzake): 'Nitakuua!'" (7:27)
Umuhimu wa elimu na toba ya haraka
Jambo la kwanza Allah alilomfundisha Nabii Adam ni majina ya vitu vyote, jambo ambalo linadhihirisha umuhimu wa elimu na kuhamasisha kuitafuta.
"Na akamfundisha Adam majina ya vitu…" (2:31). Hii pia inaonyesha umuhimu wa kuheshimu wataalamu na watu wenye elimu. Aidha, kisa kinafundisha umuhimu wa kuleta toba ya haraka, ambapo mwenye dhambi anapaswa kujuta, aache dhambi, na aombe msamaha. "Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake;" (2:37).
Unyenyekevu na madhara ya majivuno
Unyenyekevu unaonyeshwa kupitia kutii kwa Malaika amri ya Allah ya kumsujudia Adam. "Basi Malaika wakat'ii wote pamoja…" (38:73). Hii inatufundisha kuwa unyenyekevu ni njia ya kuwa karibu na Allah na waja wake.
Aidha, kisa kimetaja madhara ya kiburi: "Na kumbuka wakati tuliposema kwa Malaika: 'Msujudieni Adam.' Wakasujudu isipokuwa Ibilisi. Alikataa na alijivuna, na akawa miongoni mwa makafiri." (2:34).
Hii inatufundisha madhara ya kiburi na kujivuna, na jinsi kutomtii Allah kunavyoweza kumleta mtu katika hali ya kushindwa. Kadhalika, kisa kinataja namna Allah Mtukufu alivyomkosoa Adam na mkewe kwa kutoshikamana na amri ya Mola, lakini walikiri dhambi zao. Hii inadhihirisha umuhimu wa uwajibikaji wa maadili, kwamba kila mtu anawajibika kwa matendo yake.
Licha ya kutubu na Allah kuwasamehe, walilazimika kutoka peponi. "Na akamwambia Mola wake: 'Je, sikukuonya kuhusu mti huu, na nikakuambia kwamba shetani ni adui wazi kwenu?'" (7:22)
Subira katika utekelezaji majukumu
Mtu katika dunia hii anapitia mitihani isiyokoma, na anahitaji msaada wa subira ili kufuata amri za Allah, kadhalika subira katika kujiepusha na makatazo yake, na kustahimili kile anachokutana nacho kwa ajili ya Allah.
Kila wakati subira inapokuwa ngumu, mtu anapaswa kukumbuka baba yake Nabii Adam namna alivyotolewa peponi hadi duniani ili aendelee kuwa na subira.
Kuridhika na kudhibiti vishawishi
Shetani hakuridhika na riziki (hadhi) aliyojaaliwa na Allah, na aliona hadhi ya Adam ambayo Allah alimpatia, hivyo alimhusudu, na hiyo ikawa sababu ya uovu wake wa milele.
Hii inatufundisha kuwa ni muhimu kujifunza kuwa na moyo wa kuridhika na riziki uliyojaaliwa nayo, na pia kujiepusha na wivu na husuda.
Kisa cha Nabii Adam pia kinatufundisha umuhimu wa kuelewa vichocheo vinavyomshawishi mtu katika maisha yake. Kufuata matamanio ya nafsi na hatua za shetani ni njia ya maangamizi. Haya ni mafundisho ya malezi katika kudhibiti nafsi, kuepuka matamanio ya moyo, na kuzingatia miongozo ya kisharia.