Watoweka kwa siku 70, familia zinaendelea kuwatafuta

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro
Dar es Salaam. Kijana Gwakisa (27) Hobokela mkazi wa Tabata Kisiwani na Kelvin Montana Mushi (19) wa Mbezi Luis jijini Dar es Salaam wametoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa zaidi ya siku 70, familia zikihaha kuwatafuta.
Kelvin na Gwakisa wametoweka tangu Januari 24 na 26 mwaka huu katika matukio mawili tofauti.
Familia ya Kelvin inadai kijana wao alikwenda shuleni, hakurudi nyumbani huku begi lake la madaftari likikutwa darasani siku kadhaa tangu alipopotea.
Upande wa Gwakisa alitoweka nyumbani Januari 26, 2025 saa 3:30 usiku akiaga kuwa anakwenda kutembea nje na kuahidi atarejea baada ya muda mfupi.
Matukio yalivyokuwa
Kwa mujibu wa Regina Merchiory ambaye ni mama mzazi wa Kelvin amesema siku ya tukio, kijana wake huyo alikwenda shuleni na hakurudi.
“Ilipofika saa moja usiku, Kelvin hakuwa amerudi nyumbani, nikampigia madam simu kumuuliza akasema shuleni kulikuwa na sherehe, hivyo alichelewa.
Amesema saa mbili usiku alimpigia tena simu madam, kumueleza kwamba kijana huyo bado hajarudi nyumbani na kama ana taarifa zozote.
“Aliniambia itakuwa ni foleni tu, lakini hadi asubuhi hakuwa amerudi nikampigia tena nikamwambia naenda hukohuko shule ili nijue pa kuanzia kumtafuta,” amesema.
Amedai kijana wake ni mwanafunzi anayerudia mitihani ya kidato cha nne katika shule ya Brothers Academy iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa shule hiyo, Robert Lwezaura amesema kijana huyo si mwanafunzi wao kwa kuwa hajasajiliwa.
Amesema usajili shuleni hapo umefungwa Februari 28 na kati ya waliosajiliwa, Kelvin hayumo hivyo hawamuhesabu kama mwanafunzi wao.
"Hii shule ni ya watahiniwa wa kujitegemea, wanasoma watu wa rika tofauti, na mwanafunzi hafuatiliwi kama ameingia darasani au la, ni ‘open school," amesema.
Akifafanua kuhusu Kelvin, amesema hakuwa amelipa ada ambayo hulipwa kila mwezi, hivyo hawamuhesabu kama mwanafunzi wao kwa kuwa hadi usajili unafungwa Februari 28, Kelvin hakuwa amesajiliwa katika orodha ya wanafunzi wanaotakiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Kuhusu taarifa za kupotea, Mkurugenzi wa shule amesema amesikia, lakini hajapotelea shuleni hapo.
“Hapa shuleni tunahudumia watu wanaosoma na kurudi majumbani wa rika tofauti, hii ni shule huria, kuhusu huyu kijana kwanza sikuwa na taarifa zake kama kapotea.
“Siku napata taarifa walikuja polisi wakiongozwa na OCD (Kamanda wa Polisi Wilaya) wa Stakishari na huyo mama wakitaka kujua mazingira ya upoteaji wake, mimi sikuwa najua lolote, ndipo kuna mwanafunzi alisema ameokota begi lake darasani, akaulizwa begi liko wapi, akasema analo,” amesema.
Amesema kabla ya kwenda shuleni na polisi, aliambiwa mama huyo aliwahi kwenda shuleni na kufoka akiwaambia wafanyakazi pale kwamba watasema mwanaye alipo na lazima aifunge shule.
“Kumbe huko awali huyu mama aliwahi kutoa taarifa zake kwa mwalimu wa taaluma kwamba kijana huyo aliwahi kupotea kabla hajajiunga shuleni kwetu, hivyo akaomba walimu wamsaidie, lakini hakutaka kulisema hili baada ya kijana wake kupotea tena.
“Siku alipokuja na polisi shuleni, mwalimu wa taaluma alisema, polisi walipomuuliza kuhusu hilo akakubali, na hapa shuleni vipindi vikiisha hakuna mwanafunzi anayekuja kuaga kwa kuwa hii ni shule huria na wanafunzi wetu ni watahiniwa wa kujitegemea,” amesema.
Ingawa mama huyo amedai Februari 4,2025 alipiga simu tena shuleni kujua kama wana taarifa zozote za kijana wake, ndipo akaambiwa begi la mtoto wake limeonekana darasani.
“Hizo taarifa niliambiwa baada ya mimi kuuliza, ikabidi niende kwa mtendaji wa Ukonga kutoa taarifa, nikaripoti na Kituo cha Polisi Stakishari, ambako napo sikufanikiwa,” amesema.
Amesema polisi wa Stakishari walikwenda na kuwahoji wanafunzi watatu, mmoja alidai alimuona siku ya mwisho hiyo Januari 24 akiwa darasani kisha akatoka kwenda kununua ‘energy drink’, mwingine alidai yeye aliokota begi lake darasani, akalipeleka hosteli na mwingine alisema hajamuona Kelvin shuleni miezi mitatu.
Mmoja wa askari wa Stakishari, jina limehifadhiwa aliiambia Mwananchi kwamba Regina alifungua jalada la kupotelewa na kijana wake huyo kituoni hapo.
“Tulikwenda shuleni ambako mtoto alikuwepo, tulionana na uongozi wa shule na kupata changamoto za mtoto ambazo kimsingi mama hakutaka kuziweka wazi, hata hivyo tunaendelea na uchunguzi.
“Ila inavyoonekana huyu mtoto yupo, siku aliyopotea kuna uwezekano alikwenda njia tofauti, kwani wapo wanafunzi waliomuona wakati akiondoka shuleni, tunaendelea na uchunguzi wetu kuhakikisha anapatikana.
Upande wa Gwakisa
Kaka wa Gwakisa, Uswege Hobokela amesema mdogo wake alitoka nyumbani Jumapili Januari 26, 2025 saa 3:30 usiku akiaga kuwa anakwenda kutembea nje na kuahidi atarejea baada ya muda mfupi.
Hobokela amesema walishangaa kuona saa zikizidi kwenda bila ya kumuona Gwakisa na kuamua kumuulizia kwa majirani bila ya mafanikio yeyote, hivyo kutoa taarifa Kituo cha Polisi Tabata ambako walifunguliwa taarifa.
Pia, amesema hata baada ya kutoa taarifa bado wameendelea kumtafuta katika maeneo mbalimbali ikiwemo hospitalini pamoja na vituo mbalimbali vya polisi bila ya mafanikio yeyote.
“Tumepita katika hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana na Mwananyamala bila ya mafanikio yeyote na sasa zinatimia siku sabini tangu alipotoweka nyumbani,”amesema.
Akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kupotea kwa watu kunahitaji uchunguzi wa kina na wenye umakini ili kuzuia ufanyaji wa kazi kwa ‘presha’.
"Watu wanapotea kwa sababu mbalimbali ambazo zinahitaji uchunguzi kwa umakini, la sivyo unaweza kufanya kazi kwa ‘presha’ ili kuwaridhisha watu na mwisho wa siku ukajikuta unabambikia kesi wasiohusika," amesema Muliro.
Amesema wamekuwa wakifanya uchunguzi kwa umakini, kwani kwa kesi ambazo wamezifuatilia zaidi ya 37 wamebaini sababu kadhaa ikiwepo kisasi kwa watu ambao wamewadhulumu, ambapo baadhi yao wanabebwa na watu hao na wanapohoji familia wanadai ametekwa.
Pia, ameongeza kuwa wengine wanapotea kwa imani za kishirikina na hilo huwa linagundulika baada ya kufanyika kwa uchunguzi na kupatikana kwa watu hao.
"Wakati mwingine kuna watu wanajitambulisha kwa nafasi ya vyombo vya dola na watu wanabaki na rekodi ya kuchukuliwa na vyombo hivyo, lakini pia wapo wanaopotea kwa imani za kishirikina na wanatoa taarifa hizo wanapopatikana," amesema.
Kutokana na hilo Muliro amesema wanaendelea kufanyia kazi kila tukio linaloripotiwa polisi ili kuhakikisha watu wanakuwa salama pamoja na mali zao.
Imeandikwa na Mariam Mbwana, Imani Makongoro na Devotha Kihwelo