Watanzania watakiwa kutoogopa kutumia umeme jua

Muktasari:
- Watanzania waaswa kutoogopa gharama za awali za mfumo wa umeme jua kuwa matumizi ya nishati hiyo yana faida nyingi, ikiwemo uhakika wa kupata umeme muda wote, tena bila kulipia gharama za matumizi za kila mwezi.
Dar es Salaam. Watanzania waaswa kutoogopa gharama za awali za mfumo wa umeme jua kuwa matumizi ya nishati hiyo yana faida nyingi, ikiwemo uhakika wa kupata umeme muda wote, tena bila kulipia gharama za matumizi za kila mwezi.
Hayo yamesemwa jana usiku na Ephraim Kimati Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Compact Energies, katika tuzo za watoaji wa huduma bora za nishati ya umeme jua (ACOYA), zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Mara nyingi watu huogopa zile gharama za mwanzo za kupata umeme jua, ambazo huonekana kuwa kubwa, lakini baada ya hapo, matumizi huwa ni ya zaidi miaka 20 au 30 bila gharama nyingine zozote,”amesema na kuongeza;
“Niwahimize Watanzania kutumia mfumo wa umeme jua kwa sababu sio gharama, ila unasaidia kuokoa gharama,” amesema Kimati.
Kwa mujibu wa Kimati, mwelekeo wa dunia kwa sasa ni kutumia mfumo wa umeme jua na gesi na kwamba nchi nyingi barani Ulaya, Afrika zikiwemo zile za G7, zinasisitiza matumizi ya nishati hiyo ili kuleta maendeleo ya haraka hasa katika maeneo ya vijijini.
“Dunia sasa hivi inabadilika kuelekea nishati mbadala, ndiyo maana vitu vingi vinavyotengenezwa sasa vinatumia nishati mbadala,” amesema mkurugenzi huyo.
Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kununu huduma hizo zinazotolewa na kampuni za wazawa kwa lengo la kukuza soko la ndani, maendeleo ya nchi na kukuza nguvu ya uchumi kwa nchi za Afrika ili kushindana katika soko la dunia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Estern Star Consulting Group inayoandaa tuzo hizo, Deogratius John, amesema lengo la kuanzisha tuzo hizo ni kutambua ushindani wa kibiashara wa Afrika kwa kampuni za Afrika ili zipate utambulisho kwenye soko la dunia.
Alisema ushindi wa tuzo hizo unazifanya kampuni kuaminika katika soka na kuonyesha uwezo wao wa kutoa huduma.
John alisema ana imani kampuni za Tanzania na Afrika kwa ujumla na kwamba zina uwezo wa kushindana na kampuni za nje zilizowekeza katika teknolojia, licha ya biashara inayofanyika ndani ya Afrika ni ndogo, ukilinganisha na biashara ambayo Marekani au China inafanya na nchi za Afrika.
Tuzo hizo zimehusisha kampuni na mashirika kwenye vipengele zaidi ya 80 na ASA Microfinance wamekuwa vinara wa tuzo hizo.