Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watano wafariki dunia katika matukio matatu tofauti

Muktasari:

  • Vifo hivyo vimetokana na matukio ya wachimbaji kufukiwa na kifusi, wengine wakifariki kwa ajali, na mmoja akidaiwa kuuawa na mumewe kwa kile kinachoelezwa na Jeshi la Polisi kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Mikoani. Watu watano wamefariki dunia katika matukio matatu tofauti yaliyotokea jana na leo, Aprili 5, 2026.

Vifo hivyo vimetokana na matukio ya wachimbaji kufukiwa na kifusi, wengine wakifariki kwa ajali, na mmoja akidaiwa kuuawa na mumewe kwa kile kinachoelezwa na Jeshi la Polisi kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Musoma, mkoani Mara, wachimbaji wawili wamefariki dunia huku wengine wawili wakiokolewa baada ya kufukiwa na kifusi walipokuwa wakichimba dhahabu katika machimbo ya wachimbaji wadogo yaliyopo katika Kijiji cha Kataryo.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, Aprili 4, 2026, akisema mbali na wachimbaji hao kufariki na wengine kuokolewa, pia mmoja bado hajulikani alipo, hivyo juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Amesema tukio hilo limetokea wakati wachimbaji hao watano walipoingia katika duara (shimo) moja kwa ajili ya kufanya shughuli zao, ndipo kifusi kuporomoka na kuwafukia wakiwa ndani.

“Taarifa za awali zinasema walikuwa watu watano, na baada ya tukio wawili wametolewa wakiwa hai, wawili wakiwa wamefariki, na mmoja bado hajapatikana, juhudi za kumtafuta zinaendelea,” amesema.

Chikoka amesema shimo lililohusika katika ajali hiyo ni miongoni mwa mashimo yaliyowekewa alama kwa ajili ya kuzuia kazi za uchimbaji kutokana na masuala ya kiusalama, lakini wachimbaji hao walifanya shughuli zao kinyume cha utaratibu.

Katika tukio jingine, mkoani Arusha, watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kutoka Idara ya Kilimo na Mifugo--- Lucas Kafuru na Joshua Mwenda, wamefariki dunia kwa ajali iliyotokea leo, Aprili 5, 2026, wakiwa kazini. Taarifa ya awali ya vifo hivyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu, Juma Hokororo.

Kwingineko, mkoani Morogoro, Janet Mazengo (52), ameuawa kwa kuchinjwa, kisha kichwa chake kufukiwa shambani na mtu anayedaiwa kuwa mumewe, katika Kijiji cha Mkuruzi kilichopo Wilaya ya Kilosa.

Mtuhumiwa wa mauaji hayo, Amos Zacharia (65) maarufu Mgogo, anashikiliwa na Polisi katika kituo cha afya Ulaya baada ya kunywa sumu akijaribu kujiua baada ya kufanya mauaji hayo.

Diwani wa Kata ya Ulaya, Ally Kibati, amesema tukio hilo limetokea usiku wa Aprili 4 katika Kijiji cha Mkuruzi, Kata ya Ulaya, na kwamba mtuhumiwa alikuwa ni mzee kanisa kijijini hapo. Baada ya kufanya mauaji, alidaiwa kwenda kukifukia kichwa cha mkewe shambani.

“Baada ya kiwiliwili cha mwanamke huyo kuonekana, wananchi na vyombo vya usalama walifanikiwa kukipata kichwa kikiwa kimefukiwa shambani,” amesema Kibati.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, amesema chanzo ni wivu wa kimapenzi, kwani mtuhumiwa alikuwa akimshuku mkewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine kijijini hapo.

“Mtuhumiwa alimuua mke wake kwa kumkata shingoni na kitu chenye makali. Kwa sasa Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine, linaendelea na uchunguzi, wakati mtuhumiwa akiwa tukiwa tunamshikilia kituo cha afya Ulaya baada ya kujaribu kujiua,” amedai.