Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi yaonya wanaozusha wanaume kuibiwa nyeti, watano wafariki

Msemaji wa Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limeonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika katika kusambaza taarifa hizo au kuchochea vurugu atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limewaonya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaosambaza taarifa za uzushi kuhusu madai ya wanaume kupoteza sehemu zao za siri baada ya kushikwa bega, likisema taarifa hizo hazina ukweli wowote wa kisayansi na zimechochea vifo vya watu watano na majeruhi kadhaa.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumamosi Aprili 4, 2026, Msemaji wa Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime, imeeleza jeshi hilo limeanza uchunguzi na msako mkali dhidi ya walioanzisha na kusambaza uvumi huo.

Amesema uvumi huo umeibuka katika mikoa ya Songwe, Mbeya na Dar es Salaam, ukihusishwa na imani za kishirikina na mihemko ya wananchi, hali iliyosababisha baadhi ya watu kushambuliwa kwa tuhuma hizo. “Tunasisitiza kuwa taarifa hizi hazina ukweli wowote. Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa wanaodai kupoteza sehemu zao za siri walipokaguliwa walikutwa wakiwa kawaida kabisa,” amesema Misime.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matukio ya awali yaliripotiwa Aprili 1, 2026 katika eneo la Tunduma mkoani Songwe, yakisababisha vifo vya watu watano na wengine wawili kujeruhiwa.

Baadaye, matukio kama hayo yaliripotiwa katika eneo la Makongolosi jijini Mbeya, ambapo watu wawili walijeruhiwa, kabla ya kuenea hadi maeneo ya Kimara Mwisho na Mbezi Shule jijini Dar es Salaam Aprili 3, 2026.

Polisi imeeleza kuwa leo Jumamosi pia kumekuwa na matukio mawili mapya mkoani Mbeya yaliyosababisha watu wawili kujeruhiwa, huku madaktari wakithibitisha kuwa hakuna mabadiliko yoyote kwa wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo.

Misime ameonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika katika kusambaza taarifa hizo au kuchochea vurugu atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha kuamini na kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho, badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Wananchi wanapaswa kuwa watulivu na kutojihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ambavyo vinaweza kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia,” amesisitiza.