Vibanda 500 vyateketea kwa moto Simu 2000 Dar
Muktasari:
- Zaidi ya vibanda 500 vyateketea kwa moto stendi ya Simu 2000, mashedi sita yaliyojengwa na Halmashauri ya Ubungo yakinusurika,katika ajali hiyo hakuna kifo wala majeruhi aliyeripotiwa kuumia.
Dar es Salaam. Zaidi ya vibanda 500 inaelezwa vimeungua katika Stendi ya Simu 2000 iliyopo Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, huku mashedi sita yaliyokuwa yamejengwa na Halmashauri na vibanda 280 vikinusurika.
Tukio hilo limetokea leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, ambapo moto huo kwa mujibu wa mashuhuda ulianza saa 10 kuelekea 11 jioni.
Mwananchi iliyofika stendi hapo saa 12 jioni ilikuta tayari shughuli za uokoaji zikiendelea, huku baadhi ya wafanyabiashara ambao moto haujafika kwenye vibanda vyao wakipambana kutoa bidhaa zao ndani.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Joswph Chacha amesema walipata taarifa ya kutokea kwa ajali hiyo saa 11 jioni na kwa kushirikiana na vikosi vya Mbweni, Lugalo na Ilala walifanikiwa kutoa mitambo kwa ajili ya kwenda kuudhibiti moto huo, licha ya hadi wanafika zaidi ya nusu ya vibanda vilivyokuwepo hapo vilikuwa vimeungua.
"Kwa tathmini ya haraka hadi sasa zaidi ya vibanda 500 vimeungua huku 280 vikinusurika na mashedi sita," amesema Kamanda Chacha.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, katika vibanda hivyo kulikuwa na mchanganyiko wa biashara ambazo zimejengwa kwa malighafi ya mbao, jambo lililochangia moto kusambaa kwa haraka.
"Hata hivyo, pamoja na kutokea kwa ajali hii, tunashukuru hakuna majeruhi wala kifo zaidi ya kuteketea kwa mali," amesema Kamanda Chacha.
Kutokana na hilo, Kamanda huyo ametoa rai ya kujengwa kwa vibanda ambavyo si rahisi kushika moto, lakini pia kuwepo na vikinga moto ambavyo ajali itakapotokea vitasaidia moto kutosambaa maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, amesema baada ya kumaliza shughuli ya uzimaji moto wataanzisha uchunguzi kubaini nini hasa kilisababisha moto huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ambaye alifika eneo hilo muda mfupi baada ya kutokea kwa ajali hiyo na kushuhudia shughuli za uokoaji zinavyoendelea, amewashukuru wananchi na wafanyabiashara kwa ushirikiano wao katika kuuzima moto huo.
Kutokana na hilo, amesema wanatambua kuna wafanyabiashara waliokuwa njiani kupeleka bidhaa sokoni hapo, ambapo aliwataka viongozi wa wafanyabiashara kushirikiana na Jeshi la Polisi kuona wapi wataziweka.
Kwa wale walioharibikiwa na mali zao, Msando amesema bado ni mapema sana kusema nini watafanya kwao na kuwaomba wawe na subira.
Hata hivyo, kwa waliojenga vibanda katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo kwenye barabara za waenda kwa miguu, aliwataka kuondoka wenyewe na kueleza kuwa kila mmoja anajijua aliye katika maeneo hayo na wasingependa kutumia nguvu katika kuwaondoa.
Walichoeleza mashuhuda
Omar Mangungu, mfanyabiashara wa vinywaji sokoni hapo, amesema moto huo ulianza kuwaka eneo ambalo kuna mwenzao anafanya biashara ya kuuza mashuka na maduveti.
"Ni kutokana na aina ya bidhaa alizokuwa anauza mwenzetu ambapo moto ulipotokea uliweza kusambaa haraka kwa kuwa nyingine zina sponji ndani yake," amesema.
Naye Doto Ally amesema anasikitika moto huo umetokea ikiwa ni siku mbili tangu walipohamishiwa eneo hilo wakitokea mwisho wa soko ili kupisha ujenzi.
"Unaweza ukahisi kuna ushirikina au mipango ya siri, maana mimi na baadhi ya wenzangu tulikuwa kule mwisho ambapo moto haukufika, lakini ndiyo hivyo ajali wanasema haina kinga," amesema Doto, ambaye anasema kwa ajali hiyo amepoteza zaidi ya Sh2 milioni za bidhaa za vinywaji alizokuwa ameweka.
Apolonia Ngowi, mfanyabiashara wa pochi, amesema jana ndiyo alikuwa ameingiza mzigo wa Sh600,000 na wakati moto unatokea alikuwa amemwachia jirani yake amuangalizie kwani alikwenda kwenye maombi, na kujikuta kashindwa kuokoa chochote huku akidai amepata hasara ya Sh milioni nane kwa hesabu za haraka.
Apolonia ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwatengenezea mazingira rafiki ya kuweza kuendelea na biashara zao sokoni hapo kwa kuwa ndiyo shughuli wanayoitegemea katika kuendesha maisha yao ya kila siku na familia zao.