Watalii tisa kutoka Qatar kupanda Mlima Kilimanjaro
Muktasari:
- Watalii hao wametua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) saa 1:35 asubuhi leo Juni 16, 2025 kwa ndege ya Qatar Airways kutoka Doha, Qatar.
Dar es Salaam. Kikundi cha watalii tisa kutoka chuo cha Al Wakra Qatar Academy cha nchini Qatar, kimewasili nchini Tanzania kwa ajili ya safari yao ya tatu ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
Watalii hao wametua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) saa 1:35 asubuhi leo Juni 16, 2025 kwa ndege ya Qatar Airways kutoka Doha, Qatar.
Ujumbe huo unaongozwa na Abdirahman Handule, Mkuu wa Masuala ya Wanafunzi kutoka katika chuo hicho, na unajumuisha wanafunzi sita, mwalimu mmoja na mzazi mmoja.
Kama sehemu ya mchango wao kwa jamii, kikundi hicho pia kitazuru shule ya msingi ya Serikali katika Wilaya ya Moshi Vijijini, ambako watashiriki shughuli za kubadilishana tamaduni za jamii mbalimbali za eneo hilo na wanafunzi pamoja na walimu wa shule hiyo.
Handule ameeleza furaha yake kuhusu safari hiyo akisema: “Safari hii haileti tu changamoto za kimwili kwa wanafunzi wetu, bali pia inawapa uzoefu wa kielimu na kitamaduni wa kubadilisha maisha. Tunajivunia kuendeleza utamaduni huu wa kujifunza na kuhudumia mataifa.”
Safari hiyo ya kipekee ni sehemu ya dhamira pana ya taasisi hiyo katika elimu ya nje ya darasa, ukuzaji wa uongozi na kukuza uhusiano ya kitamaduni kati ya mataifa.
Pia, ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri kati ya Ubalozi wa Tanzania mjini Doha na Al Wakra Qatar Academy, kufuatia mafanikio ya safari mbili za awali za kupanda Mlima Kilimanjaro.
Mara walipowasili, walipokelewa kwa furaha na Godwill Kyegeko, Ofisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kuanzia Juni 16 hadi 25, 2025, kundi hilo la watalii limepanga kupanda hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika.
Mbali na safari ya kupanda mlima, watashiriki pia katika shughuli mbalimbali za kujifunza kuhusu urithi wa asili na utamaduni wa mkoa huo kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, kijiji cha kitamaduni cha Wamasai (Masai Boma), Maporomoko ya Maji ya Materuni, na mashamba ya kahawa mkoani Kilimanjaro.