Wasomi wataja tiba kumaliza migomo ya wafanyabiashara

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Picha na Aurea Simtowe

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Mei 15, 2023 waligoma hadi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoingilia kati kuuzima. Wakagoma tena Juni 24, 2024. 

Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi wameshauri njia zinazoweza kutumika kumaliza migomo inayojirudia ya wafanyabiashara nchini, wakipendekeza kufanyika utafiti wa kina utakaosaidia kutungwa sera ya namna ya kufanya biashara.

Pia wamehimiza kuaminiana, kufanya makadirio ya kodi yaliyo ya haki na yanayolipika na kuwapo majadiliano.

Wameeleza hayo kutokana na mgomo wa wafanyabiashara uliodumu kwa takribani siku nne katika maeneo kadhaa nchini ukianzia Kariakoo, Dar es Salaam, Juni 24, 2024.

Ni kutokana na mgomo huo, Serikali imeondoa ukomo wa faini ya juu ya kosa la kutotoa risiti za kielektroniki (EFD) ya Sh15 milioni na badala yake kuweka Sh4 milioni.

Faini hiyo ilikuwa miongoni mwa sababu ya kuwapo mgomo wa wafanyabiashara pamoja na malalamiko ya kukamatwa katika ukaguzi unaofanywa mara kwa mara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hatua ya kupunguza faini ilitokana na majadiliano ya takribani siku nne kati ya Serikali na Jumuiya ya Wafanyabiashara iliyotoa madai na hoja takribani 41.

Baada ya vikao na mawaziri wa sekta husika, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alihitimisha mazungumzo hayo, wakiafikiana kusimamia maazimio 15.

Si mara ya kwanza kwa wafanyabishara wa Kariakoo kugoma, Mei 15, 2023 mgomo mkubwa ulifanyika uliodumu kwa siku tatu mfululizo hadi pale Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoingilia kati kwa kukutana na wafanyabiashara hao kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.

Aliambatana na mawaziri saba wa kisekta, wakiwamo Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba; Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji; Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Kamishna wa TRA.

Waziri Mkuu Majaliwa alisikiliza kero za wafanyabiashara hao ambazo zingine alizitolea majibu. Pia aliunda kamati ya kutatua mgogoro baina ya wafanyabiashara hao na Serikali iliyojumuisha wajumbe 14.


Maoni ya wachumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini nchini (Repoa), Dk Donald Mmari, amesema ni vyema Serikali ikakaa na wafanyabiashara na kuwasikiliza kitu gani wanahitaji.

Amesema sekta binafsi ndiyo injini ya nchi, hivyo ni vyema kuwasikiliza kuelewa nini wanachokihitaji na wao waeleze wanachokihitaji.

Ameshauri kila kitu kipangwe katika hali iliyo ya haki, hususani kodi, uingizaji wa bidhaa kutoka nje, tathmini, makadirio ya kodi, na utozaji kodi.

“Pia viwango vya kodi vitozwe kulingana na mzunguko wa biashara, ubia kati ya sekta binafsi na Serikali inahitaji kuaminiana na kila kitu kifanyike kwa uwazi,” amesema Dk Mmari.

Mchambuzi na mtaalamu wa uchumi, Dk Donath Olomi, amesema migomo inayofanyika ina athari za moja kwa moja na hali ikiendelea hivyo inaweza kusababisha kupoteza wateja na hasa baada ya kupata eneo lingine la kununua bidhaa, akitoa mfano wa soko linalojengwa Ubungo.

“Suala lingine linalopaswa kuangaliwa ni lile la machinga kukaa barabarani na kuuza mali sawa na wamiliki wa maduka, huku wakiwa hawalipi kodi ya pango, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na tozo za huduma,” amesema.

Hali hiyo amesema hufanya baadhi ya wenye maduka kuamua kuuza bidhaa kupitia migongo ya machinga na kugawana fedha.

Mtaalamu wa uchumi na biashara, Profesa Aurelia Kamuzora amesema kinachoweza kumaliza suala hilo ni kufanyika utafiti na tathmini ya kina kujua wafanyabiashara wanataka nini.

Tathmini hiyo amesema itawezesha kutungwa sera ambazo zitatoa mwongozo wa namna ya ufanyaji biashara, upangaji wa wafanyabiashara na ukusanyaji wa mapato.

“Pia bodi zilizopo zitumike ipasavyo, tunaamini waliopo wana uwezo wa kufanya kazi vizuri, ikishindwa iwajibishwe, wasikwepe majukumu yao, kwani yenyewe ina uwezo wa kufanya tafiti na kujua kinachoendelea,” amesema.

Mchambuzi wa uchumi, Oscar Mkude amesema kuwapo kwa meza ya majadiliano kunapotokea mvutano kati ya wafanyabiashara na mamlaka na kutokuwapo mtu anayeonekana kuwa msemaji wa mwisho katika kila kitu husika,  ni moja ya njia ya kuondoa migomo.

“Kilichokosekana ni nafasi ya watu kukaa na kujadiliana, watu wanakuwa kama wanataka kukwepa majadiliano, lakini ni jambo ambalo linatakiwa kufanyika kwa sababu kila mtu ana mawazo yake na kila mtu awe tayari kupokea mawazo ya mwenzake,” amesema.

Amewataka watendaji wa Serikali kuwa wazi na kusikiliza sekta binafsi wanachotaka na kinyume chake, akishauri kutokuwapo mabishano ya ubabe.

“Kama Serikali inakuja na kodi mpya lazima izungumze na walengwa, ikiwa katika hatua za awali, tofauti na kinachofanyika maoni yanakwenda kuchukuliwa wakati ambao upitishaji wa muswada au bejeti uko hatua za juu jambo linalofanya maoni mengine kuchukuliwa bajeti inayofuata, hapa katikati watu wanakuwa wameumia,” amesema.

Ameshauri kuwapo mrejesho kwa wafanyabiashara kuhusu kilichofanyiwa kazi baada ya malalamiko kutolewa na iwapo kimeshindikana zitajwe sababu wajue kuliko kukaa kimya.

Mgomo huo uliathiri mnyororo mzima wa biashara, ukihusisha wafanyabiashara wenyewe, wateja na watoa huduma zingine kama vile wasafirishaji mizigo, makuli, watoa huduma za kifedha na wauza vyakula.

Serikali pia kwa upande wake ilikosa mapato.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Kaimu Mkurugenzi Elimu Kwa Mlipakodi na Mawasiliano, Hudson Kamoga imeliambia Mwananchi:

"Ninachoweza kusema mgomo wa Kariakoo uliathiri shughuli za ukusanyaji wa mapato ya kila siku unaofanywa na TRA."