Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgomo wa kufungua maduka wafika Mwanza, Mbeya

Baadhi ya maduka ya simu katika mtaa wa Msimbazi yakiwa yamefunguliwa leo Jumanne Juni 25, 2024. Picha na Devotha Kihwelo

Muktasari:

  • Machinga wahaha kusaka bidhaa, baadhi ya wateja wahamia maeneo mengine.

Dar/Mikoani. Wakati mgomo wa wafanyabiashara eneo la Kariakoo, Dar es Salaam ukiingia siku ya pili leo, umeungwa mkono na wengine wa mikoa ya Mbeya na Mwanza.

Hata hivyo, katika maeneo hayo, baadhi ya wafanyabiashara wamefungua maduka na kuendelea na biashara kama kawaida.

Kuendelea kufungwa kwa maduka katika eneo la Kariakoo, mbali ya kuwaathiri wateja, pia wachuuzi wameeleza kukwama kupata bidhaa.

Kutokana na hilo, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameamua kufuata mahitaji katika maeneo mengine, likiwamo Soko la Tandika ambako pia wapo baadhi ya wafanyabiashara waliofunga maduka.

Mgomo unaendelea licha ya jana, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo kutangaza kusitishwa kazi ya ukaguzi wa risiti za kielektroniki (EFD) na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Mkoa wa Kikodi Karikaoo.

Serikali imefikia hatua hiyo, wakati ikiandaa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo katika Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo.

Profesa Mkumbo alisema katika kikao cha viongozi wa wafanyabiashara na Serikali kilichofanyika juzi, wamekubaliana kuwapanga machinga, ili kutoingilia ufanyaji biashara wa wenye maduka na kuhakikisha kila anayefanya biashara analipa kodi kama ilivyokubalika.

Kabla ya mgomo huo, kulisambazwa vipeperushi kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, viongozi wa wafanyabiashara walisema hawakuutangaza, wakiwasihi wanachama wao kuendelea na biashara kwa kuwa wapo Dodoma kwa ajili ya vikao na Serikali.

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Picha na Aurea Simtowe

Wamtaka Rais Samia

Baadhi ya wafanyabiashara eneo la Kariakoo leo Jumanne Juni 25, 2024 wamesema wanataka Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kusikiliza malalamiko yao.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, wamechoshwa na matamko ya viongozi walio chini yake, wakidai hakuna utekelezaji wa yaliyofikiwa na kikosi kazi kilichoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwaka 2023 walipogoma.

Katika eneo la Kariakoo, tangu leo alfajiri hadi saa 3.30 asubuhi maduka mengi yalikuwa yamefungwa, huku wauzaji hawakuwapo tofauti na jana walipokuwa nje ya maduka yao.

Nassor Ally, mfanyabiashara wa Kariakoo amesema Rais pekee ndiye anayeweza kutatua matatizo yao.

“Mawaziri wamekuja hapa, Waziri Mkuu amekuja hapa hakuna kitu, imeundwa kamati hakuna kilichofanyika tukakiona, aje Rais atusikilize labda atatuelewa kwa sababu walio chini yake wameshindwa,” amesema Ally na kuongeza kuwa tamko kuzuia kamatakamata si mara ya kwanza linatolewa.

Mfanyabiashara Mahmoud Mussa amewalalamikia polisi akidai wamegeuka kuwa maofisa tathmini na ukaguzi, hivyo kuwa kero.

“Mtu unamkagua mzigo anakupa risiti unasema risiti haiendani na mzigo, wewe ndiyo umemuuzia, umetumia kigezo gani kusema thamani ya mzigo haiendani na mzigo? Inakera, polisi wasimame kwenye kazi zao na si kuingilia biashara,” amesema Mussa.


Biashara ya machinga

Tofauti na jana, wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga waliotumia fursa ya kufungwa maduka kufanya biashara, leo wameeleza kukosa bidhaa kutokana na wamiliki wa maduka kuyafunga.

“Serikali iwasikilize yaishe, aje Rais wanayemtaka hali ni mbaya, kuna wafanyabiashara wengi kutoka nje wako hapa kutoka Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC) na Zambia wamekwama hawajapata mzigo, sisi wenyewe unapata mteja hauwezi kwenda kuchukua mzigo tunakosa hela,” amesema Mussa Juma.

Amesema kufunguliwa maduka ndiko kunachangamsha biashara kwa kuwa wanaishi kwa kutegemeana na hasa wanapopata wateja wanaoshindwa kuwahudumia.

Muuza nguo za ndani, Lucky Isack amesema mgomo unaiathiri zaidi Serikali kwa kupoteza mapato.

"Jana tumekaa tukaondoka Serikali haijaingiza kodi yoyote," amesema.


Maduka yafunguliwa

Wafanyabiashara wa simu wameendelea na biashara zao kama kawaida.

Muuza simu Mtaa wa Msimbazi, Asha Salum amesema wamefungua duka kwa sababu kodi ya pango inakaribia kuisha, hivyo wakifunga hawatapata fedha za kulipia.

"Malalamiko yaliyotolewa ni ya msingi na yanatugusa wote, lakini kwa upande wetu ni ngumu kwa sababu tunahitaji kulipa kodi inayoisha mwezi huu, nikifunga sitaingiza pesa yoyote kwa sasa," amesema.

Amesema tofauti na wafanyabiashara wa bidhaa nyingine, wao wanachangia watu zaidi ya wanne dukani, hivyo ni vigumu kufunga.


Wafuata mahitaji Tandika

Katika Soko la Tandika kumekuwa na msongamano wa watu kwa kiasi kikubwa wakiwa kinamama.

Baadhi ya waliozungumza na Mwananchi wamesema imewalazimu kufuata mahitaji sokoni hapo kutokana na hofu ya kukosa bidhaa za mahitaji ya shule.

"Jumatatu watoto wanakwenda shule, sasa huu mgomo wa wafanyabiashara umenishtua, nimeona niwahi bidhaa za watoto mapema nisijenunua kwa bei ghali baadaye," amesema Maimuna Said, mkazi wa Keko Mwanga, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wachuuzi wamesema changamoto iliyopo ni upatikanaji wa bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wengi wamefunga maduka.

Mchuuzi, Eliya Mbaga amesema wateja wengi wanahitaji bidhaa za shule zaidi wakati huu ambao shule zinaenda kufunguliwa.

Amesema anauza madaftari, viatu, soksi, sare za shule na mabegi.

"Upatikanaji wa bidhaa unaweza ukawa na changamoto siku za usoni kutokana na wafanyabiashara wakubwa kufunga maduka. Ila tunaamini Serikali imesikia kilio chao, watatekeleza, ili biashara iendelee maana sisi tunategemea kupata bidhaa kutoka kwao," amesema.

Baadhi ya maduka sokoni hapo yamefungwa, huku mengine yakiendelea na biashara.

Bila kutaja majina, waliofungua maduka wamesema hakuna tangazo rasmi walilolipata, hivyo wameona waendelee na biashara kama kawaida.

Maduka katika soko la Kabwe jijini Mbeya yakiwa yamefungwa baada ya mgomo wa wafanyabiashara. Picha na Saddam Sadick

Mkoani Mbeya.

Jijini Mbeya mgomo imeanza leo

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mbeya (JWT), Charles Syonga amethibitisha kuwapo mgomo huo, akieleza uongozi haujaelekeza wafanye hivyo.

"Uongozi haujaelekeza chochote kwa mtu yeyote kufunga duka, tunajua changamoto zipo kama kodi na tozo mbalimbali, lakini kero zote zilishawasilishwa serikalini, tunasubiri agizo la mamlaka za Serikali," amesema.

"Tunawaomba warejeshe huduma wakati huu Serikali ikiendelea kulifanyia kazi suala hili," amesema.

Kabla ya jana wamiliki wa maduka katika Soko la Mwanjelwa walifunga biashara kabla ya Serikali kuingilia kati.

Hali ilivyo Mwanza

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati amesema wapo waliofunga maduka wakilalamikia sheria za kodi.

“Malalamiko na matamanio ya wafanyabishara ni kuona sheria zinazosimamia wafanyabiashara zimerekebishwa,” amesema.

Uamuzi wa kufunga maduka umewaathiri machinga na wachuuzi wa bidhaa kutoka mikoa ya jirani na Mwanza.

Mchuuzi kutoka wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, Enock Timba amesema alifika jijini hapo saa 12.30 asubuhi kununua bidhaa akaishia kuzunguka bila kuona duka lililofunguliwa.

“Sikutarajia nitakuta mgomo, nimeathirika inabidi nizunguke sijui maduka yamefunguliwa wapi. Hata hivyo, ninakoelekea sasa ni kurudi nyumbani sioni dalili za maduka kufunguliwa,” amesema.

Mkazi wa Nyasaka jijini humo, Maria Nzemba amesema hofu yake ni namna gani atarejesha mkopo aliochukua kwa ajili ya kuanzisha biashara, akisema amekosa bidhaa za kuzungusha mtaani katika eneo lake.

RPC aahidi ulinzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema baada ya kufanya doria katika mitaa ya Jiji la Mwanza, ikiwemo ya Rwagasore, Kaluta, Uhuru, Liberty, Nyamagana na Miti Mirefu wamebaini si wafanyabiashara wote waliogoma kufunga maduka.

Kutokana na hilo, amesema maofisa wa Jeshi la Polisi wenye sare na wasio na sare wapo mitaa kuimarisha ulinzi kwa waliofungua maduka.

“Wasiwe na hofu ya aina yoyote ulinzi umeimarishwa katika viunga vyote vya Mkoa wa Mwanza, askari wanafanya doria za magari na miguu, wako tayari kumdhibiti atakayewafanyia vurugu wafanyabiashara waliokubali kufungua maduka,” amesema. Kamanda Mutafungwa.


Vyama vya siasa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema ili Serikali isitishe kuongeza kodi kwa wafanyabiashara, mikoa mingine inapaswa pia kufunga biashara.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, akizungumza katika mkutano wa operesheni +255KatibaMpya Kanda ya Kaskazini, uliofanyika eneo la Minjingu, wilayani Babati mkoani Manyara amesema anatamani wafanyabiashara waendelee kufunga maduka, ili Serikali ipunguze gharama za kodi kwani bila hivyo bidhaa zingepanda bei zaidi.

“Waliosoma hawana ajira hata wenye biashara ndogo wanakamuliwa na TRA wanaumizwa na ugumu wa maisha na haya mambo hayana muujiza wowote. Namna pekee ya kulikomboa Taifa ni wananchi kujiunga na Chadema, kushiriki chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani," amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema jana kuwa wanaunga mkono mgomo wa wafanyabiashara.

Akizungumza akiwa Monduli alisema wanaunga mkono kwa kuwa Tanzania mifumo mingi ya kikodi inaua mitaji ya wafanyabiashara na kuwakosesha matumaini ya kuendelea. 

“Tunawaunga mkono wafanyabiashara wa Kariakoo na nawaomba wafanyabiashara wengine Tanzania nzima tufike mahali kupigania uchungu wa maisha yetu. Kinachofanya Kariakoo ni faida kwa Taifa hili,” alisema.

Kwa upande wake, Mwanaisha Mndeme, Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa ACT-Wazalendo katika taarifa kwa vyombo vya habari leo amesema Serikali itamke kisheria kuwa eneo la Kariakoo ni eneo huru za biashara.

“Tunaitaka Serikali kuweka mazingira rafiki kwa machinga na makundi mengine ya walalahoi kutumia maeneo mbalimbali ya miji katika kujiingizia kipato na kuinua maisha yao.

ACT-Wazalenno imewataka wafanyabiashara kuwa na mshikamano usioyumba kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa kikamilifu,” amsema.


Imeandikwa na Aurea Simtowe, Dovetha Kihwelo, Herieth Makwetta, Saddam Sadick, Mgongo Kaitira, na Janeth Mushi