Wateja Dar wahamia Soko la Tandika

Muktasari:
- Upatikanaji wa bidhaa pia huenda utaanza kuwa changamoto siku za usoni kutokana na wafanyabiashara wakubwa kufunga maduka
Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya maduka kufungwa katika Soko la Tandika, wachuuzi wa bidhaa ndogondogo na wateja wamehamia sokoni hapo.
Maduka hayo yamefungwa kutokana na mgomo wa wafanyabiashara ulioingia siku ya pili leo Juni 25, 2024 ukianzia eneo la Kariakoo.
Katika Soko la Tandika kumekua na msongamano wa watu, kwa kiasi kikubwa wakiwa kina mama.
Baadhi ya waliozungumza na Mwananchi Digital wamesema imewalazimu kufuata mahitaji sokoni hapo kutokana na hofu ya kukosa bidhaa za mahitaji ya shule.
"Jumatatu watoto wanaenda shule, sasa huu mgomo wa wafanyabiashara umenishtua, nimeona niwahi bidhaa za watoto mapema nisijenunua kwa bei ghali baadaye," amesema Maimuna Said mkazi wa Keko Mwanga jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wachuuzi wamesema changamoto iliyopo ni upatikanaji wa bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wengi wamefunga maduka yao.
Mchuuzi, Eliya Mbaga amesema wateja wengi wanahitaji bidhaa za shule zaidi wakati huu ambao shule zinaenda kufunguliwa.
Amesema anauza madaftari, viatu, soksi, sare za shule na mabegi.
"Upatikanaji wa bidhaa pia huenda utaanza kuwa changamoto siku za usoni kutokana na wafanyabiashara wakubwa kufunga maduka. Ila tunaamini Serikali imesikia kilio chao, watatekeleza ili biashara iendelee maana sisi tunategemea kupata bidhaa kutoka kwao," amesema.
Baadhi ya maduka sokoni hapo yamefungwa, huku mengine yakiendelea na biashara.
Pasipo kutaja majina, waliofungua maduka wamesema hakuna tangazo rasmi walilolipata, hivyo wameona waendelee na biashara kama kawaida.