Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanufaika na teknolojia ya kilimo shadidi

Mkuu wa wilaya ya Kilombero Danstan Kyobya (katikati) akizungumza na wakulima akiwa kwenye shamba la mfano la kilimo Shadid cha mpunga wakati wa maadhimisho ya siku ya mkulima iliyofanyika wilayani humo, kulia ni katibu tawala wilaya hiyo Abrahim Mwaikwila na kushoto ni mkulima kiongozi wa kilimo hicho Shadidi Salumu Balakasa. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Kilimo Shadidi kimeleta manufaa kwa wakulima kwa kuwa kinahitaji mbegu chache, kinatoa mavuno mengi na kinachangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Ifakara. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kituo cha Ifakara, inaendelea kunufaisha wakulima kwa kutoa elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora za mpunga na mbinu za kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kilimo Shadidi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Siku ya Mkulima uliofanyika katika kijiji cha Katurukila, kata ya Mkula, Halmashauri ya Mji wa Ifakara leo Jumamosi Julai 5, 2025, mtafiti wa mbegu bora za mpunga kutoka Tari, Theodor Thomas amesema teknolojia ya Kilimo Shadidi imeleta tija kubwa kwa wakulima kwa kuwa inahitaji mbegu, maji kidogo na eneo dogo la shamba lakini inatoa mavuno mengi.

Aidha, Thomas amesema teknolojia hiyo inasaidia kupunguza hewa ukaa ambayo ni chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri sekta ya kilimo na mazingira kwa ujumla.

Thomas amesema mafunzo kuhusu Kilimo Shadidi yalianza kutolewa kwa wakulima tangu mwaka 2023 katika maeneo ya Kilombero, Mbarali (Mbeya), Bunda, Ruvu, Kilosa, Njage na Malinyi.

Amebainisha kuwa lengo ni kuwawezesha wakulima kutumia rasilimali kidogo lakini kupata mavuno mengi.

“Mbali na faida za kiuchumi, kilimo hiki kinachangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, hivyo ni rafiki kwa mazingira,” amesema Thomas.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amesema katika kata ya Mkula tayari kuna kundi la vijana wapatao 40 ambao wameanza kutumia teknolojia hiyo na wameweza kupata kipato.

“Tunahitaji teknolojia hii iwafikie vijana wote wa Ifakara wanaojishughulisha na kilimo. Nawaagiza maofisa maendeleo ya jamii kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri inawafikia vijana hawa walioamua kujikita kwenye kilimo,” amesema Kyobya.

Hata hivyo amesema amefurahishwa na ushiriki wa viongozi wa vijiji na vitongoji ambao wamekuwa mfano kwa wakulima kwa kukubali teknolojia hiyo, ambayo inamwezesha mkulima kuvuna mara tatu hadi nne kwa mwaka.

“Tukiadhimisha Siku ya Mkulima, tunasherehekea pia ujio wa teknolojia hii ya kisasa. Ni rafiki kwa mazingira kwa sababu inatumia eneo dogo, maji kidogo na mbegu chache, lakini inatoa mavuno mengi,” amesema Kyobya.

Mwenyekiti wa kijiji cha Katurukila na mkulima wa mfano, Salum Balakasa ameeleza jinsi alivyofaidika na teknolojia hiyo.

Amesema kabla ya kutumia Kilimo Shadidi, alikuwa akivuna magunia mawili hadi matatu ya mpunga kwenye shamba lake lenye ukubwa wa karibu hekari mbili. Sasa anavuna magunia 10 hadi 13 kutoka shamba hilohilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya (aliyechuchumaa) akisikiliza maelezo kutoka kwa mkulima kiongozi wa kilimo Shadidi cha mpunga Anna Maganga (aliyeinama) kwenye sherehe ya siku ya mkulima iliyofanyika wilayani humo. Picha Hamida Shariff

Balakasa amekiri kwamba awali alipinga teknolojia hiyo, lakini baada ya kuona mafanikio ya wenzake, naye aliamua kujaribu na kupata mavuno mengi kuliko hapo awali.

Naye mkazi wa kijiji cha Katurukila, Joseph Melkior ameishukuru Tari kwa elimu wanayoendelea kuitoa kwa wakulima kuhusu u Kilimo Shadidi.