Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake watahadharishwa rushwa ya ngono kuelekea Uchaguzi Mkuu

Muktasari:

  • Watakiwa kuripoti wanapokutana na changamoto ikiwemo kuombwa rushwa ya ngono ili hatua zichukuliwe kwa wahusika kwa mujibu wa sheria, lengo likiwa kuwafanya wanawake wengi kujitokeza kuwania nafasi za uongozi bila kukutana na vikwazo.

Dar es Salaam. Ikiwa imesalia miezi minane kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, wito umetolewa kwa wanawake kutambua kwamba tatizo la rushwa ya ngono linaweza kuwa kikwazo, hivyo wawe tayari kukabiliana nalo katika mchakato wa kugombea na kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Sambamba na hilo, wanawake wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali kupitia uchaguzi huo wametakiwa kusimama imara na kutosita kuripoti kwa mamlaka husika wanaposhawishiwa kutoa rushwa ya ngono ili kupata nafasi.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Februari 5, 2025 na Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben wakati wa uzinduzi wa Jarida la Sauti ya Siti linaloandaliwa na chama hicho likiwa limebeba ujumbe kuhusu rushwa ya ngono katika vyombo vya habari.

Dk Rose amesema suala la rushwa ya ngono siyo la kufumbiwa macho kwa kuwa linakatisha ndoto za wanawake wengi hivyo wanapaswa kujiandaa kukabiliana na udhalilishaji huo ili kuruhusu kundi hilo kuingia kwa wingi kwenye nafasi za maamuzi.

“Tumeingia mwaka wa uchaguzi, wanawake wanapaswa kufahamu kwamba rushwa ya ngono ipo ila hawapaswi kuikubali kama kikwazo, wanatakiwa kupambana nayo kwa kuwa inadhalilisha utu, wajue kwamba kuna sheria inawalinda hivyo wawe makini kuweka vielelezo kuwashtaki wanaoweka katika mazingira ya rushwa ya ngono.

Mkurugenzi wa Tamwa Dk Rose Reuben (kulia) na mwakilisho wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) Paulina Teveli wakionesha toleo jipya la jarida la Sauti ya Siti lenye maudhui kuhusu rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari.

“Kwa upande wetu Tamwa tutaelimisha jamii ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo wanawake watakaowania kwenye nafasi mbalimbali na kuwajengea uwezo wale wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema Dk Rose.

Ameongeza kuwa; “Pia tutatukuwa tunafuatilia ni kwa namna gani vyombo vya habari vinaandika habari za wagombea wanawake ikiwa ni pamoja na kurekodi matokeo ya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono yatakayotokea kipindi hiki kueleke uchaguzi.”

Akizungumzia Jarida la Sauti ya Siti ambalo limebeba maudhui ya hali ya rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari, Dk Rose amesema kwa sasa umeanza kuonekana unafuu kwa kuwa waathirika wameanza kuvunja ukimya na kueleza yanayowakabili.

“Miaka ya michache iliyopita tulikuwa na changamoto ya ukimya kuhusu vitendo hivi, sasa hivi tunaona hali hiyo inabadilika na waathirika wanazungumza na hata kwenye jarida kuna simulizi za waathirika. Kwetu hii ni hatua kubwa kuanza kuona watu wanazungumza,”amesema Dk Rose.

Mwakilishi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), Paulina Teveli amesema kutolewa kwa jarida hilo ni hatua katika mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji wa wanawake.

“Rushwa ya ngono ni tatizo ambalo halipaswi kufumbiwa macho kwenye vyombo vya habari, hili lilionekana kuwa kikwazo kwa wanahabari wengi wanawake na wapo waliolazimika kukimbia fani, hivyo tunapoona jitihada za aina hii zinafanyika inaleta matumaini makubwa,” amesema Paulina.