Wanawake wapewa mazingira wezeshi sekta ya madini

Mkurugenzi wa Anglo Gold Ashanti, Simon Shao akizungumzakatika Jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika Machi 8, 2024 katika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam leo. . Picha Michael Matemanga
Muktasari:
- Makamu wa Rais kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Anglo Gold Ashanti, Simon Shayo amesema wana viongozi wakuu wanawake na wameona tofauti kubwa katika tija na ushiriki wao.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Anglo Gold Ashanti, Simon Shayo amesema ili kuongeza idadi ya wanawake katika sekta ya madini wameweka mazingira wezeshi kuhakikisha wanapewa kipaumbele katika ajira na nafasi za uongozi.
Shayo amesema hayo leo Ijumaa, Machi 8, 2023 katika maadhimisho ya Jukwaa la The Citizen Rising Women linalofanyika jijini hapa likiwa na kauli mbiu isemayo: “Wekeza kwa wanawake, ongeza kasi ya maendeleo.”
Makamu huyo wa Rais wa Anglo Gold Ashanti ambayo imedhamini jukwaa hilo kwa miaka minne, amesema ari ya kuendelea kufadhili inaongezeka kwa kuwa kuna mengi yanaibuliwa na vyombo vya habari, hivyo ni fursa nzuri kukuza uwezo wa wanawake.
Amesema sekta binafsi kama ilivyo ya umma kuna uchache mkubwa kwenye uwezeshaji wa wanawake.
“Tafiti zilifanywa, wenzetu Canada wana asilimia 16 tu wanawake katika sekta ya madini, hivyo tukijilinganisha sisi tumepiga hatua kupitia majukwaa kama haya kuunganisha fikra kuna uwakilishi na ushiriki kwa wanawake na pia kuwanyanyua wengine waone inawezekana.
“Kampuni yetu ‘group chair’ ni mwanamke, viongozi watatu kati ya saba wakuu ni wanawake, nikiri hapa kwamba tangu tumekuwa na viongozi wakuu wanawake tumeona tofauti kubwa katika tija na ushiriki wao,” amesema.
Shayo amesema ushiriki wa wanawake katika kampuni hiyo wamepiga hatua kwa kuwa na asilimia 23, hivyo wanahakikisha kuna ushiriki wa wanawake hata katika nafasi ambazo wanaume wanashiriki.
“Tunahakikisha asilimia 50 ya wanaoingia kutoka vyuo vikuu ni wanawake au wasichana, upembuzi kwa walioomba kazi ni lazima iwe 50 kwa 50 na iwapo wamefungana kwa sifa tunamchukua mwanamke.
“Katika miaka mitatu au minne hatukuwa huko, lakini katika kampuni yote sisi tuna wanawake wawili kwenye uongozi wa juu wa kampuni na tunaamini nafasi tulizokalia sisi miaka michache ijayo tutawapisha wanawake wenye sifa,” amesema Shayo.
Shayo amemshukuru Rais kuendelea kuonyesha njia kwa kuwa wameona baraza la mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Sisi tuna kampeni kubwa mbili, moja inasema usivuke mstari kwetu ukimshika mwanamke hata bega inakuondoa kazini siku hiyo hiyo, hata waliposema sasa tutapataje wenza tulisema kuna wenza kwa kwenda kwa stara,” amesema.
Pia, amesema kuna kampeni ya paza sauti, inayotaka kila aina ya unyanyasaji za kijinsia uripotiwe, “na tukijua mmoja amenyanyasa kijinsia tungependa kuachana naye salama bila kujali jinsia yake wala hali yake.”