Hii hapa siri SBL kufikia asilimia 42 wanawake katika uongozi

Dr Obinna Anyalebechi, Managing Director of Serengeti Breweries Limited (SBL) akizungumza katika Jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika Machi 8, 2024 katika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam leo.
Muktasari:
- Katika nafasi za uongozi wa Kampuni ya SBL asilimia 42 ni wanawake na lengo ni kufikia asilimia 50 mpaka kufikia 2030.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited, Obinna Anyabelechi amesema sera ya kampuni hiyo inawataka hadi kufikia mwaka 2030 katika nafasi za uongozi kuwe na wanawake asilimia 50.
Anyabelechi amesema hayo leo Ijumaa Machi 8, 2024 katika Kongamano la ‘Rising Woman’ lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) lenye lengo la kuwainua wanawake katika jamii.
“Na kwa Tanzania hadi leo, katika nafasi za uongozi wa kampuni yetu (SBL) asilimia 42 ni wanawake na lengo ni kufikia asilimia 50 mpaka kufikia 2030,”amesema Anyabelechi.
Aidha, kampuni hiyo ni tanzu ya sehemu ya Kampuni ya East Africa Brewries Limited kupitia kwa mkurugenzi wake, imesema ina mkakati wa ujumuishi katika uongozi unaochochea usawa huo.
“Kimataifa tuna ndoto mpaka kufikia 2030 asilimia 50 ya nafasi zote za uongozi ziwe chini ya wanawake, hivyo kwa upande wa Tanzania pia ina ‘target’ malengo ya ambayo nimepangiwa ya kuifikia katika usawa,” amesema na kuongeza Anyabelechi.
Akizungumzia jinsi ya kuifikia asilimia 50 ya viongozi wanawake, Anyabelechi amesema ni pamoja na kuwa na mkakati mzuri wa udahili wa kuajiri viongozi unaowasaidia wanawake na kutengeneza mazingira bora ya kazi ya wanawake kazini.
“Unahitaji kuwa mikakati bora inayowanufaisha wanawake katika mchakato wa ajira na kwa upande wetu tunahakikisha katika wale wanaoomba kazi watakaopata nafasi ya kuitwa kwa mahojiano na asilimia 50 lazima wawe wanawake,” amesema.
Pia, ameongeza kuwa njia nyingine ni kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kazini ikiwamo ruhusa ya uzazi.
Katika kongamano hilo la Rising Woman linalofanyika katika ukumbi wa The Super Dome Masaki, mgeni Rasmi ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.