Wanawake wafunguka kukomesha udhalilishaji Mirerani

Wadau wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wakifuatilia mdahalo wa ushiriki imara wa wanawake katika shughuli za madini ulioandaliwa na CSP.  Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Awali, wanawake wadau wa madini Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, walikuwa wanavuliwa nguo ili kupekuliwa ila sasa wanakaguliwa kwa stara, kituo cha polisi kina askari na uchongaji wa barabara umefanyika

Mirerani. Wanawake wadau wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameona matokeo chanya kwenye shughuli zao kwani hivi sasa hawapekuliwi kwa kudhalilishwa na kuvuliwa nguo.

Wanawake hao walikuwa wanapekuliwa kwa kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo, ila baada ya kulalamikia hali hiyo kwenye mdahalo ulioandaliwa na Shirika la Civic Social Protection Foundation (CSP) hivi sasa matokeo chanya yameonekana.

Mwanasheria wa CSP, Eliakim Paulo akizungumza kwenye mdahalo wa ushiriki imara wa wanawake katika shughuli za madini kwenye eneo la machimbo ya madini Mirerani Oktoba 30 amesema hali imebadilika.

Paulo amesema hivi sasa wanawake wadau wa madini wanatumia fursa ya madini ya Tanzanite kufanya shughuli zao tofauti na awali walikuwa wanakutana na vikwazo vingi ikiwemo udhalilishwaji.  

Amesema wanawake hao walikuwa wanapekuliwa kwa kuvuliwa nguo ila hivi sasa wakiwa kwenye chumba cha upekuzi wanapekuliwa kwa ustaarabu na siyo kudhalilishwa tena.

Amesema mradi huo umepata mafanikio kwani hata kituo cha polisi machimboni na kitengo cha dawati la jinsia linafanya kazi hivyo malalamiko ya wadau wanawake yamefanyiwa kazi. 

“Hata barabara ya kwenda kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite, imechongwa na kampuni ya Franone Mining, hivyo magari na pikipiki wanatumia bila vikwazo tofauti na awali,” amesema Paulo.

Hata hivyo, amesema bei ya matumizi ya vyoo nayo imeshushwa kwani awali ilikuwa Sh1,000 na hivi sasa ni Sh500 ila bado mazungumzo yanaendela ili nauli za pikipiki za kubeba abiria (bodaboda) washushe nauli kutoka Sh2,000 hadi Sh1,000.

“Suala la mabasi madogo bado lipo kwenye mazungumza ili magari ya kubebea abiria ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite, yaruhusiwe kufanya kazi,” amesema Paulo.

Mmoja kati ya wanawake wadau wa madini ya Tanzanite, Fatuma Kifunta amesema upekuzi usiokuwa na stara ulikuwa unawakwaza kwani ulikuwa unakiuka haki za binadamu.

"Tunashukuru mno kwani mradi huu wa CSP umekuja na matokeo chanya kwani hivi sasa udhalilishwaji uliokuwa ukifanyika awali umekoma kwani hivi sasa watu wanapekuliwa kistaarabu," amesema.

Mdau mwingine Hawa Kiranga ametoa wito kwa serikali kuhakikisha vyombo vya moto vya usafiri ikiwemo mabasi madogo yanaruhusiwa ili kuwarahisishia usafiri wanawake wajasiriamali.

Kiranga amesema magari ya abiria yakiwa ndani ya ukuta wa madini itakuwa nafuu kwa wajasiriamali kwani nauli itakuwa Sh500 na kunufaisha watu wengi hasa wasio na kipato.