Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanavyuo 17 kortini wakidaiwa kughushi nyaraka kupata mkopo wa HESLB

Muktasari:

  • Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 47, tukio wanalodaiwa kutenda  kati ya kati ya Juni 2024 hadi Novemba 2025 katika Jiji la Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Watu 18 wakiwemo wanafunzi 17 wa vyuo vikuu na mhitimu mmoja, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka 47 yakiwemo ya kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za uongo na kujipatia mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa hao kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Bahari Dar es Salaam (DMI), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) na Chuo Kikuu cha Kairuki (KU), wamefikishwa Mahakamani hapo leo Juni 12, 2026 na kusomewa kesi ya jinai namba 13088 ya mwaka 2026.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni wanafunzi wa IFM, Frank Kayamba, Eline Urio, Brian Kessy na Loveness Mrutu; Wanafunzi wa CBE, Sophia Macha, Elias Kasiga na Silass Daniel pamoja na Clara Nyarusai, ambaye ni mwanafunzi wa UDSM.

Pia, mwanafunzi wa NIT Eva Namjuzi; mwanafunzi wa DMI Nyasilu Magadula na Badru Lenga; na wanafunzi wa MNMA, ambao ni Aziza Bashiru, Anitha Godfrey, Cyprian Champunga na Elneth Nyagawa.

Wengine ni mhitimu wa NIT, Idrisa Omary; mwanafunzi wa DIT Mohamedi Sefu na mwanafunzi wa KU, Michael Shoide.

Wamesomewa mashtaka yao na mawakili wawili wa Serikali, Titus Aaron na Cathbert Mbilingi kwa kupokezana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.

Akiwasomea mashtaka yao, Wakili Aron alisema mshitakiwa wa kwanza hadi wa 15 kila mmoja alikuwa akikabiliwa na mashtaka matatu; mshtakiwa Shoide yeye anakabiliwa na mashtaka manne na Omary, huku Sefu akikabiliwa na  mashtaka 16.

Inadaiwa kuwa, kati ya Juni 2024 hadi Novemba 2025 washtakiwa wote wakiwa na nia ovu ya kudanganya waliandaa nyaraka za uongo za ulemavu kupitia mfumo wa maombi ya mkopo ya elimu ya juu (OLAMS).

Iliendelea kudaiwa kuwa walifanya hivyo kwa lengo la kuonyesha kuwa wao na wengine wazazi wao wana ulemavu, wakati wakijua si kweli.

Pia, ilidaiwa kuwa kati ya tarehe hizo mshitakiwa Kayamba, Sophia, Clara, Eline, Kessy, Loveness, Kasiga, Eva, Silass, Magadula, Lenga, Aziza, Anitha, Champunga, Elneth na Shoide waliwasilisha nyaraka hizo kwa lengo la kuonesha wao na wengine wazazi wao ni walemavu.

Katika mashitaka ya kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu, Kayamba, anadaiwa kupata mkopo wa Sh5.85 milioni kwa kudai kuwa baba yake ana ulemavu, huku Champunga akidaiwa kupata Sh5.89 milioni kwa madai kama hayo.

Mshtakiwa Sophia, Eline, Kessy, Loveness, Eva, Magadula na Lenga wanadaiwa kila mmoja kujipatia Sh2.2 milioni kupitia mikopo hiyo kwa kutumia taarifa za uongo.

Iliendelea kudaiwa kuwa, Urio anadaiwa kujipatia Sh2.8 milioni,  Daniel Sh2.217 milioni, Anitha Sh2.195 milioni, Elneth, Jonathan, Nyagawa Sh2.15 milioni, Clara Sh1.8 milioni na Aziza Sh1.785 milioni, baada ya kuwasilisha nyaraka hizo za uongo.

Washitakiwa hao wanadaiwa kufanya vitendo hivyo kwa nia ya kudanganya na kujinufaisha kwa kupata mikopo kutoka HESLB.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mbuya aliwauliza washitakiwa hao kama ni kweli au si kweli kuwa walitenda makosa hayo lakini washtakiwa wote walikana kuwa si kweli.

Pia, upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na waliomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja zao za awali(Ph).

Pia, Jamhuri walidai kuwa mashtaka hayo yanadhaminika hivyo aliieleza Mahakama itakavyoona inafaa iwawape masharti ya dhamana.

Hakimu Mbuya, alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao ambayo ni kila mtu awe na kitambulisho.

Pia, kila mshtakiwa alitaki kujidhamini yeye mwenyewe kwa kutumia vitambulisho vya chuo na kusaini bondi ya Sh3 milioni kila mmoja.

Kuhusu mshtakiwa wa 16, yeye  alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja.

Hakimu Mbuya, alitoa masharti mengine ni kuwa washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi.

Vilevile, hawatakiwi kusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, isipokuwa kwa ridhaa ya Mahakama.

Pia, alimtaka mshitakiwa wa kwanza ambaye ni Kayamba kupeleka mdhamini wa kumdhamini kabla hajamaliza chuo kwani baada ya kumaliza kitambulisho chake hakitokuwa na kazi.

Kesi iliahirishwa hadi Julai 9, 2026 kwa ajili ya kusomwa hoja za awali (PH).

Washtakiwa wametimiza masharti ya dhamana na kuachiwa kwa dhamana.