Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga alivyojitetea kortini

Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama (aliyejifunika shuka) akiwa na aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo, Sibuti Nyabuya ( mwenye t-shirt nyeupe) pamoja na mfanyabiashara, Joseph Mpangala (mwenye shati la dark blue) wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, baada ya kusomewa hoja za awali katika kesi ya kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa na kujipatia Sh 45 milioni. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Hii ni kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga na wenzake wawili wanaodaiwa kughushi barua ya Msamaha wa Rais, akionyesha imetolewa kwa wafungwa watatu raia wa China na kujipatia Sh45milioni.

Dar es Salam. Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Josephat Mkama ameieleza Mahakama hakuna ushahidi uliyowasilishwa mahakamani kuonyesha alighushi barua ya nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru, ya Desemba 21 mwaka 2022.

Mkama ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kughushi msamaha wa rais kwa wafungwa inayomkabili yeye na wenzake wawili, ametoa utetezi wake, leo Jumatano Juni 10, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kujitetea.

Inadaiwa Mkama na wenzake wawili walifanya hivyo kwa lengo la kuonyesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa nyongeza ya msamaha wa Rais kwa wafungwa watatu raia wa China mwenye namba 585/2019 Song Lei, 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin

Mbali na bwana jela, washtakiwa wengine ni Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa Gereza la Ukonga na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, ambao wote wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 25517/2024.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu raia wa China, wenye namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.

Inadaiwa Machi 18, 2016 wafungwa watatu wenye asili ya China, ambao ni mfungwa namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliohukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo katika Gereza la Ukonga.

Wafungwa hao walihukumiwa vifungo tofauti kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali na wote walikuwa hawajuani.

Hata hivyo, Desemba 21, 2022, Mkama kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa gereza hilo na Nyabuya ambaye alikuwa ofisa Tehama wa gereza hilo kwa kipindi hicho, walitengeneza nyaraka ya kughushi  yenye kichwa cha habari ‘'Nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru.

Nyaraka hiyo ambayo ni barua ya Desemba 21, 2022, iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.

Alitoa ushahidi wake, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, Mkama amedai  upande wa mashtaka hawakuwahi kuleta shahidi yeyote aliyeithibitishia Mahakama kuwa yeye ndiye aliyeghushi barua hiyo na pia hakuna shahidi aliyedai kuwa alimuona wakati anaghushi barua hiyo.

Mshtakiwa huyo ametoa ushahidi dhidi ya mashtaka manne yanayomkabili kipindi hicho akiwa mkuu wa gereza hilo.

"Mheshimiwa hakimu, wafungwa hao (raia wa kigeni) hawakuwahi kufika mahakamani na kusema kuwa walimpa Sh45 milioni kwa ajili ya kushughulikia barua hii," amedai Mkama na kuongeza:

"Hakuna shahidi wa upande wa mashtaka aliyefika mahakamani kuleta simu au kamera kuonesha kwamba mimi nilifanya mawasiliano na mshtakiwa wa kwanza na wa pili (Sibuti Nyabuya na Joseph Mpangala) kwa ajili ya kuongoza genge la uhalifu,"amedai Mkama

Katika utetezi wake, Mkama amekiri kusimamishwa kazi kipindi akiwa mkuu wa gereza hilo, ili kupisha uchunguzi na hatua za sheria kufuatwa, lakini hakujua uchunguzi ulikuwa unafanywa na nani.

"Mheshimiwa hakimu, vitu ambavyo vilidaiwa kuchukuliwa magereza wakati nimesimamishwa kazi, havikuwahi kuletwa mahakamani na hakuna ushahidi wowote uliyoletwa na upande wa mashtaka kuwa alipokea fedha hizo, wala nyaraka za benki, wala miamala ya simu," amedai

Kuhusu tuhuma za kuwahamasisha magereza wafungwa hao baada ya tukio hilo, amedai kuwa hakuna shahidi aliyeieleza Mahakama kuwa wafungwa hao walihamishwa kwa sababu gani na pia hakuna sababu yoyote iliyoletwa mahakamani kuonesha kwa nini waliyodai kuibiwa hawakuja mahakamani.

Akijibu maswali ya dodoso ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theresia Mtao, Mkama amedai kuwa ni kweli waathiriwa walikuwa ni raia wa China na pia hawakuwahi kujua kama wana msamaha na hakuwahi kuwaita ofisini kwake.

"Kwa mujibu wa barua, nilisubiri kujua tuhuma zinazonikabili, kwa hiyo sikuona haja ya kujua nani anachunguza tuhuma zangu na pia sijawahi kupokea maelekezo yoyote kutoka wizarani kuhusiana na wahanga  (waathiriwa) hao," amedai.

Pia, amedai kuwa hana mamlaka ya kuwapangia upande wa mashtaka ni shahidi gani aletwe mahakamani.